Katika kuhakikisha kuwa watumishi wapya wa kada ya ualimu wanazingatia misingi ya utumishi bora wa umma, Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kupitia Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imeendesha mafunzo elekezi kwa  walimu wa ajira mpya 86 wa shule za msingi na sekondari walioajiliwa Mwaka 2025 katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga.

Mafunzo hayo yaliyofanyika Julai 1, 2025 yamelenga kuwajengea uwezo walimu hao ili wawe waadilifu, wazalendo, wachapakazi, na wafanye kazi kwa weledi na kuwafundisha, kuishi maisha bora pamoja na kujiepusha na vitendo viovu katika maeneo yao ya kazi, na kwenye jamii wanakoishi.


Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Idara ya Utumishi na rasilimali watu Manispaa ya Sumbawanga, Bw. Kulanga Matia Kanyanga amesisitiza juu ya uadilifu, bidii kazini, nidhamu, kujituma, pamoja na kuepuka tabia zisizofaa kama vile wizi, ulevi na mikopo isiyokuwa na tija hususani katika hatua za awali za ajira zao.


Bw. Kulanga ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kufundishia ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu na huduma za kijamii, hali ambayo imeibadilisha taswira ya Mji wa Sumbawanga kuwa wa kisasa na wa kuvutia, tofauti na simulizi potofu za awali kuwa ni kisiwa cha uchawi.
Kwa upande wake, Peter Steven Yamahi, mmoja wa walimu wapya walioshiriki mafunzo hayo, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuajiri walimu na kuwezesha mafunzo ya utumishi bora kwa vitendo. Ameeleza kuwa hatua hiyo imewasaidia kupata uelewa mpana kuhusu wajibu wao katika kuleta maendeleo ya kitaaluma kwa wanafunzi.

Mafunzo hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa walimu.