MUNGE wa Jimbo la Ilala jijini Dar es Salaam, Mussa Zungu, ameibuka kidedea katika uchaguzi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiahidi kuongoza chombo hicho kwa uwazi, nidhamu na uwajibikaji mkubwa.
Uchaguzi huo umefanyika jijini Dodoma ambapo Zungu alipata kura 378 kati ya kura zote zilizopigwa na wabunge, hatua iliyomuwezesha kushika rasmi nafasi ya Spika wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa ushindi huo, Zungu anakabidhiwa jukumu zito la kusimamia mwenendo wa mijadala, kuhakikisha utekelezaji wa majukumu ya kibunge kwa maslahi ya wananchi, na kudumisha heshima ya Bunge kama mhimili muhimu wa dola.
Katika uchaguzi huo, wagombea wengine walioshiriki ni Veronica Tyeah wa NRA, Anitha Mgaya wa NLD, Chrisant Nyakitita wa DP, Ndonge Ndonge wa AAFP, na Amin Yango wa ADC, ambapo kati yao wawili tu walipata kura moja moja huku wengine wakikosa kura kabisa.
Zungu amechaguliwa kwa kura 378 kati ya 383 zilizopigwa kutoka kwa wabunge wa bunge la Tanzania, huku kura 3 zikiharibika.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema uteuzi wa Zungu unaashiria mwanzo mpya wa uongozi wa Bunge unaotarajiwa kuweka msisitizo kwenye uwajibikaji wa Serikali na uwakilishi wenye tija kwa wananchi.

Tunapatikana Kupitia