Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ametoa wito kwa sekta binafsi kushirikiana na Vyuo, kuwekeza katika tafiti hususan za sayansi na teknolojia ili kuinua viwango vya tafiti na ubora wa elimu nchini.
 
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa uzinduzi wa mpango wa ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Waajiri, uliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Amesema Kupitia Mpango huo, sekta binafsi inaweza kuchangia maendeleo ya elimu kwa kufadhili tafiti na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa fani mbalimbali kulingana na mahitaji ya soko la ajira.
 
Aidha, Makamu wa Rais ametoa wito kwa Taasisi za elimu na Sekta binafsi nchini kuzingatia maendeleo ya kasi ya sayansi na teknolojia duniani katika utekelezaji wa Mpango huo. Amesema Vyuo na Sekta binafsi vishirikiane kubaini ujuzi muhimu unaohitajika sasa na siku zijazo hususan katika fani za sayansi, teknolojia, ubunifu, tiba, uhandisi na hesabu ili kuwezesha vijana kushindana na kupata nafasi katika soko la ajira  nchini na kimataifa.
 
Makamu wa Rais amesema ushirikiano baina ya Taasisi za elimu na Viwanda ni hitaji la lazima katika dunia ya leo, kwa kuwa Vyuo haviwezi tena kuwa visiwa vya nadharia, na viwanda haviwezi kukua bila nguvukazi yenye ujuzi unaoendana na teknolojia na ushindani wa soko.

Ameongeza kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele cha kimkakati katika kukuza ujuzi, stadi, maarifa na sifa za kuajirika au kujiajiri miongoni mwa vijana na wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu, ikitambua kwamba maendeleo endelevu ya Taifa hayawezekani bila kuwa na rasilimaliwatu iliyoelimika na yenye uwezo wa kuchangia kikamilifu katika uchumi wa Taifa.

Amesema Serikali imeendelea kufanya maboresho makubwa ya sera na mitaala ya elimu katika ngazi zote kwa lengo la kuujenga mfumo wa elimu ulio mnyumbufu, jumuishi na unaoendana na vipaji, mwelekeo na mahitaji halisi ya soko la ajira, huku ikizingatia mabadiliko ya teknolojia na ushindani wa kitaifa na kimataifa.