
RUKWA:
MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere ameahidi kuipa kipaumbele
miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ya kupeleka umeme kwenye
vitongoji 156 vya Awamu ya Pili B (HEP 2B) inayotekelezwa mkoani humo.
RC
Makongoro amebainisha hayo leo Februari 3 mara baada ya kupokea taarifa
ya utekelezaji wa mradi huo iliyowasilishwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi
Mkuu wa REA, Bw. Frank Mugogo sambamba na kumtambulisha mkandarasi
kampuni ya M/s Dieynem Co Ltd atakayetekeleza mradi huo.
"Mimi
natoa maelekezo sasa kwa watu wangu, mradi huu wa REA kwa miaka mitatu
ijayo kuanzia sasa tutaipa kipaumbele na itakuwa ni ajenda ya kudumu
katika kamati yangu ya usalama ya Mkoa ili kuhakikisha mradi
unatekelezwa vyema na kwa ubora, " amesisitiza RC Makongoro.
Kwa
upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mugogo amesema kuwa
mkoa wa Rukwa una jumla ya vitongoji 1,816, vitongoji vyenye umeme ni
1,508 na vitongoji ambavyo havina umeme ni 308.
"Kupitia mradi
wa HEP 2B vitongoji 156 vinakwenda kupelekewa umeme kwa mkoa wa Rukwa na
wateja wapatao 5,508 wataunganishiwa na huduma ya umeme. Gharama ya
kuunganisha umeme ni Sh 27,000 tu naomba mfahahamu na tuwaeleze wananchi
katika maeneo ya mradi" amesema Mugogo.
Naye, Meneja wa Miradi
wa Kampuni ya Dieynem Co. Ltd, Mha. Novatus Lyimo ameahidi kumaliza
mradi huo kwa wakati na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa za uwepo wa
mradi huo katika maeneo yao ikiwemo kutumia fursa za ajira mbalimbali
zitakazotolewa kipindi chote cha mradi.
Tunapatikana Kupitia