Wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga wameendelea kushiriki kikamilifu katika zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika leo Februari 28, 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha mji unakuwa safi, salama na wenye kulinda afya za wakazi.

Zoezi hilo limefanyika katika Soko la Mandela na kushirikisha Viongozi wa Serikali, Taasisi za Umma, Taasisi binafsi, wafanyabiashara pamoja na wananchi mbalimbali, likiwa na lengo la kuhamasisha uwajibikaji wa pamoja katika utunzaji wa mazingira.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Bw. Nassir Kirusha amesisitiza wananchi kuendeleza tabia ya kufanya usafi wa mazingira kila wakati badala ya kusubiri ratiba rasmi ya usafi wa mwisho wa mwezi.

Amesema kudumisha usafi wa mazingira ni hatua muhimu ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu, mafua makali na homa za matumbo, ambayo yamekuwa yakiripotiwa katika maeneo mbalimbali duniani, na kwamba kinga bora huanza na mazingira safi.

Aidha, amewahimiza wananchi kuzingatia afua za lishe bora sambamba na usafi wa mazingira, akieleza kuwa hatua hizo kwa pamoja zinachangia kuimarisha afya na ustawi wa jamii.

Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga inaendelea kutekeleza mikakati ya usafi wa mazingira kila siku, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya kuhakikisha mji unakuwa safi, salama na unaochochea maendeleo endelevu ya wananchi.

"Sumbawanga bila Uchafu Inawezekana"
#Tunza Mazingira Yakutunze
WEKA MJI SAFI