Wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika masoko ya Mandela, Sabasaba pamoja na wale wanaofanyia biashara kando ya barabara wametakiwa kuzingatia sheria za matumizi sahihi ya maeneo ya biashara na usafi wa mazingira, hususan katika kipindi hiki cha majira ya masika.

Akizungumza wakati wa ziara ya utoaji elimu kwa wafanyabiashara, Ndugu Gabriel Masinga Katibu Tawala wa Wilaya ya Sumbawanga amesema kuwa kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha, maji yamekuwa yakituama katika maeneo mbalimbali, hali inayoongeza hatari ya magonjwa kwa wananchi.

“Tuko kwenye kipindi cha masika, tumebarikiwa mvua nyingi. Maji yanatuama kila mahali na mengine yanaelea. Hii ni hatari kiafya, hasa kwa biashara za vyakula,” amesema.

 

Katika hatua ya kudhibiti hali hiyo, wafanyabiashara wote wanaofanya biashara kwenye hifadhi ya barabara zinazomilikiwa na TANROADS na TARURA wamepewa siku saba kuondoa na kuhamia katika maeneo rasmi yaliyotengwa kwa ajili ya biashara.

Aidha, amewataka wafanyabiashara kuzingatia kwa umakini suala la usafi, hasa wanaouza vyakula, akisema ni marufuku kuweka bidhaa kama samaki, nyanya, vitunguu, ndizi na vyakula vingine chini, kutokana na hatari ya kuathiriwa na bakteria, vimelea vya magonjwa na wadudu.


“Chakula kikigusana na maji machafu au kuwekwa chini, bakteria na wadudu wanaweza kupenya na kusababisha magonjwa kwa walaji,” ameongeza.

Mamlaka imetoa wito kwa wafanyabiashara kushirikiana na serikali katika kutekeleza maelekezo hayo kwa lengo la kulinda afya za wananchi na kudumisha usafi wa mazingira ya mji.