Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema "lina wasiwasi mkubwa" kuhusu mpango uliositishwa wa majaribio ya chanjo ya hepatitis B nchini Guinea-Bissau, likitilia shaka uhalali wake wa kisayansi na jinsi unavyolingana na viwango vya utafiti kimataifa kuhusu kushirikisha binadamu katika shughuli kama hiyo.
Utafiti uliopendekezwa ungehusisha maelfu ya watoto wachanga. Watafiti walipanga kuwapa baadhi ya watoto wachanga chanjo ya hepatitis B wakati wa kuzaliwa, na pia walipanga kuwapa watoto wengine tofauti dozi hiyo wiki sita baada ya kuzaliwa.
Lengo lilikuwa kutathmini athari za kiafya kwa jumla wakati chanjo hiyo inapotolewa pamoja na chanjo zingine za kawaida.
Hepatitis B imeenea sana nchini Guinea-Bissau, ambapo karibu mtu mmoja kati ya watu watano wazima ameambukizwa, huku karibu asilimia 11% ya watoto wadogo wakiwa wameambukizwa – hali inayowaweka watu wengi katika hatari ya ugonjwa mbaya wa ini na pia kifo.
WHO imesema iko tayari kuunga mkono Guinea-Bissau katika juhudi zake za kukabiliana na ugonjwa huo.Mwezi uliopita, waziri wa afya wa Guinea-Bissau, Quinhin Nantote, alithibitisha kuwa jaribio hilo "limesimamishwa", na sasa amewaalika wataalamu kutoka Afrika CDC na mataifa mengine duniani kuzuru taifa hilo hivi karibuni ili kusaidia mamlaka kutathmini utafiti huo uliopendekezwa.


Tunapatikana Kupitia