Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Shadrack Masija, ametoa wito kwa wananchi kuwa waangalifu wanapotumia mitandao ya mawasiliano na majukwaa ya kidijitali ili kujiepusha na vitendo vya uhalifu wa kimtandao vinavyoendelea kujitokeza katika jamii.

Kamanda Masija ametoa wito huo Machi 13, 2026 wakati akishiriki futari (iftar) iliyoandaliwa na mtandao wa simu wa Yas katika Ukumbi wa Country Hotel uliopo Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, hafla iliyowakutanisha wadau mbalimbali wa mawasiliano na wananchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, SACP Masija amesema kumekuwa na ongezeko la matukio ya uhalifu wa kimtandao ikiwemo utapeli kupitia simu na mitandao ya kijamii, ambapo baadhi ya watu hutumia teknolojia vibaya kwa lengo la kujipatia fedha au taarifa za wengine kwa njia zisizo halali.

Kutokana na hali hiyo, amewahimiza wananchi kuwa makini wanapotumia simu na mitandao ya kijamii kwa kuepuka kutoa taarifa zao binafsi kwa watu wasiofahamika pamoja na kuchukua tahadhari wanapofanya miamala ya kifedha kupitia simu.

Aidha, Kamanda Masija amesisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa pindi wanapobaini vitendo vya uhalifu wa kimtandao ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa mapema na kulinda usalama wa wananchi na mali zao.