Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa Machi 8 kila Mwaka, Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kupitia Kata za Katandala, Mazwi na Malangali imefanya ziara ya kutembelea Kituo cha Kulea Watoto Wenye Mahitaji Maalum cha Bethania Drop-In Centre Future and Hope kilichopo Kata ya Katandala, Manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa.

Pamoja na mambo mengine, msaada wa utu pamoja na kushiriki muda wa furaha na watoto hao vimefanyika, ikiwa ni ishara ya kuenzi utu, upendo na mshikamano wa kijamii katika kipindi hiki cha maadhimisho.

Aidha, katika kuimarisha uchumi wa wanawake, wajasiriamali wamepatiwa elimu kuhusu ubunifu katika biashara, malezi na makuzi bora ya watoto, pamoja na fursa zilizopo katika maeneo yao. Elimu inayolenga kuwawezesha kunufaika kikamilifu na mikopo ya Serikali isiyo na riba kwa makundi maalum, yenye lengo la kuinua wajasiriamali na kukuza maendeleo endelevu. Sambamba na hilo, wamepatiwa mafunzo ya matumizi sahihi ya kifaa cha kuzimia moto (fire extinguisher) kwa ajili ya usalama wa biashara na nyumbani.

Maadhimisho haya yameendelea kuonesha dhamira ya Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga katika kuhamasisha usawa, uwezeshaji wa wanawake na kujenga jamii yenye mshikamano.

Kupitia elimu na matendo ya utu, jamii inahimizwa kushiriki kikamilifu katika jitihada za kuwalinda na kuwawezesha wanawake na wasichana kwa maendeleo jumuishi na endelevu.

"Haki kwa Wanawake na Wasichana; Msingi wa Maendeleo Jumuishi kufikia Dira 2050"