Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Rukwa, Jacqueline Mzindakaya, amegawa kadi 30 za mfano kati ya kadi 48,500 zilizoelekezwa kugawiwa mkoani Rukwa, zikilenga watu wenye mahitaji maalum, watoto na mama wajawazito katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote.
Akizungumza leo Machi 4, 2026 katika semina iliyowakutanisha Wanachi wa lengwa wa kaya zisizo na uwezo pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani humo, Mzindakaya amesema kadi hizo zimetolewa kwa kaya masikini ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za afya bila vikwazo vya kifedha.
Katika hotuba yake, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza ahadi aliyoitoa katika siku 100 za mwanzo wa uongozi wake ya kuhakikisha Watanzania wasiojiweza wanapata bima ya afya bure. Amesema mpango huo unalenga kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na uhakika wa matibabu bila kujali hali yake ya kipato.
Mbunge huyo pia amesema Rais Samia tayari ameelekeza kiasi cha shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mikopo, ambapo wanufaika wakubwa ni wanawake, hatua inayolenga kuwawezesha kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mkoa wa Rukwa kutoka National Health Insurance Fund (NHIF), Amos Edward, amesema serikali imejipanga kuhakikisha mpango wa bima ya afya kwa wote unatekelezwa kwa ufanisi, ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa dawa katika vituo vyote vitakavyotoa huduma hiyo.
Aidha, amewakumbusha watoa huduma katika hospitali kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi bila ubaguzi, kuepuka matumizi ya lugha zisizofaa kwa wanachama wa bima ya afya na kuwahudumia kwa usawa wananchi wote, wakiwemo wanaolipia huduma kwa fedha taslimu.
Mbali na masuala ya afya, semina hiyo pia ilitoa elimu ya ujasiriamali ambapo washiriki walipata mafunzo kuhusu mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri, yaliyowasilishwa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga Noela Munis, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.

Tunapatikana Kupitia