Wananchi wa Tarafa ya Mwimbi, wilayani Kalambo mkoani Rukwa, wametakiwa kujenga imani na Jeshi la Polisi pamoja na kutoa ushirikiano wa dhati ili kusaidia kutanzua vitendo vya uhalifu katika maeneo yao. 

Wito huo umetolewa Machi 31, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Shadrack Masija, alipofanya mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mwimbi.

Akizungumza na wananchi hao, SACP Masija alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Polisi na jamii ni msingi muhimu katika kudhibiti na kuzuia uhalifu. Alieleza kuwa Jeshi la Polisi linahitaji taarifa sahihi na kwa wakati kutoka kwa wananchi ili kuwabaini wahalifu na kuchukua hatua stahiki za kisheria. Aidha, alikumbusha kuwa dhamana kwa makosa yanayodhaminika hutolewa bure, hivyo wananchi wanapaswa kuepuka kutoa au kudai rushwa katika mchakato huo.

Katika mkutano huo, Kamanda Masija pia alitoa rai kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi, akieleza kuwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kupoteza maisha au kuvuruga utulivu wa jamii. Alisisitiza kuwa kila tukio la uhalifu linapaswa kuripotiwa kwa vyombo vya dola ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.

Sambamba na hilo, alipokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusu mwenendo wa baadhi ya askari, na kuahidi kuyafanyia kazi kwa haraka ili kuhakikisha haki inatendeka na kuimarisha uhusiano mzuri kati ya Polisi na jamii. Alisisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitavumilia vitendo vyovyote vya ukiukwaji wa maadili kwa askari wake.

Mwisho, aliwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuleta maendeleo na amani katika jamii yao.