
Walimu walioajiriwa katika Utumishi wa Umma Mwaka 2025 katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga wamepatiwa mafunzo elekezi leo Machi 13, 2026 kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu Utumishi Bora na kuwasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika kuendeleza sekta ya elimu.
Kupitia mafunzo hayo, Walimu hao wamehimizwa kufanya kazi kwa bidii, kuzingatia weledi wa taaluma yao na kuongeza ufaulu wa Wanafunzi shuleni kulingana na malengo ya Serikali pamoja na matarajio ya Wazazi na Wanafunzi. Aidha, wametakiwa kuepuka tabia zisizofaa ambazo ni kinyume na Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.
Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Bw. Nassir Kirusha, ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuweka mifumo imara ya Utumishi wa Umma kupitia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali pamoja na utoaji wa Ajira Mpya kwa Watumishi.

Amesisitiza kuwa Ualimu ni Wito na Walimu ni Kioo cha Jamii, hivyo wanapaswa kuwa Walezi Bora wa Wanafunzi kwa kuzingatia Uadilifu, Nidhamu na kufanya Kazi kwa bidii ili kuwa mfano mzuri katika Jamii.
Aidha, Bw. Kirusha amewataka Walimu hao kuepuka tabia hatarishi zikiwemo mikopo umiza na badala yake kuzingatia Nidhamu ya Kazi, Uwajibikaji na Moyo wa kujituma katika kutekeleza majukumu yao.
Kwa upande wao Walimu hao wameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapatia Ajira pamoja na mafunzo hayo ambayo yamewasaidia kuongeza uelewa kuhusu Utumishi wa Umma.
Katika mafunzo hayo, Walimu wamepatiwa elimu kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo Kupambana na Kuzuia Rushwa, Utunzaji wa Siri, Bima ya Afya, Haki na Wajibu wa Walimu, Maadili na Nidhamu ya Utumishi, Muundo wa Uongozi pamoja na Utoaji wa huduma bora kwa Wananchi










Tunapatikana Kupitia