Katika kuadhimisha Siku ya Wauguzi Duniani, wauguzi Mkoani Rukwa wamejumuika leo kimkoa katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kusherehekea hatua muhimu kwa taaluma yao, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango mkubwa na wa kipekee wa wauguzi katika kuimarisha sekta ya afya Nchini.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni “UUGUZI NI NGUVU YA MABADILIKO”, ikilenga kuonyesha namna taaluma ya uuguzi inavyobeba matumaini, mabadiliko na ustawi wa jamii kupitia huduma bora za afya kwa Wananchi.
Akizungumza Mgeni Rasmi wa hafla hiyo, Katibu Tawala Msaidizi wa Divisheni ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Ibrahim Izack Mwita, amesema kuwa wauguzi wana nafasi muhimu kama mawakala wa mabadiliko chanya katika jamii kutokana na huduma zao zenye weledi, ubunifu, huruma na nidhamu ya hali ya juu.
"Wauguzi wanahusika na takribani asilimia 80 ya huduma zote za afya zinazotolewa hospitalini na kwenye vituo vya afya, huku wakiwa ni asilimia 60 ya rasilimali watu katika sekta ya afya. Hii ni ishara tosha kuwa wao ni uti wa mgongo wa huduma za afya Nchini," amesema Dkt. Mwita.
Aidha, amewataka wauguzi kuzingatia matumizi ya mifumo ya teknolojia kama Digital Health System, ili kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya kidijitali, jambo ambalo litasaidia kuongeza ufanisi, uwazi na uharaka katika utoaji wa huduma za afya.
Kwa upande wake, Muuguzi Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mazwi, Shadhir Varanga, amesema wauguzi mkoani humo wanajivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan katika sekta ya afya kupitia ujenzi wa miundombinu, ununuzi wa vifaa tiba na upatikanaji wa dawa.
"Serikali imeweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi. Leo hii tunaweza kutoa huduma kwa ufanisi zaidi, tukizingatia misingi ya taaluma yetu ya kuokoa maisha. Hili linaongeza morali ya kazi kwa wauguzi," amesema Varanga.








Tunapatikana Kupitia