Na Fedrick Mbaruku - Rukwa

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, CP Benedict Wakulyamba, ameongoza hafla ya kugawa mizinga ya kisasa ya nyuki kwa viongozi wa kimila (machifu) mkoani Rukwa, ikiwa ni sehemu ya mpango wa serikali wa kuendeleza sekta ya ufugaji nyuki na uhifadhi wa mazingira.

Hafla hiyo imefanyika Agost 19,mwaka huu katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa rukwa ambapo imewaleta pamoja machifu kutoka wilaya zote mkoani humo, ambapo jumla ya mizinga 200 imegawiwa kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Akizungumza katika tukio hilo, CP Wakulyamba amesema hatua hiyo inalenga kuongeza thamani ya sekta ya nyuki, kuimarisha upatikanaji wa mazao ya nyuki, na kuwashirikisha viongozi wa kimila katika kulinda na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wao, baadhi ya machifu waliopokea mizinga hiyo waliishukuru serikali na TFS kwa kuwajali na kuwaweka mstari wa mbele katika jitihada za kulinda maliasili, huku wakiahidi kuhamasisha jamii zao kushiriki kwa vitendo katika ufugaji nyuki na uhifadhi wa misitu.

Mmoja wa maafisa uhifadhi wa TFS, Mkoa wa Rukwa, amebainisha kuwa zoezi hilo ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa usambazaji wa mizinga ya kisasa kwa wadau mbalimbali, unaolenga kuongeza pato la wananchi na taifa kwa ujumla kupitia sekta ya nyuki.