Katika kuhakikisha afya za mifugo na kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na ufugaji, Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa imezindua kampeni ya chanjo ya ng’ombe dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu ya ng’ombe (CBPP) pamoja na uwekaji wa hereni kwa njia ya kielektroniki.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Mhe. Nyakia Chirukile, amehimiza wafugaji kuhakikisha mifugo yao inachanjwa na kuwekewa hereni ili kuboresha afya na takwimu za mifugo, hatua itakayowezesha sekta hiyo kushindana katika soko la ndani na nje ya Nchi.
Kupitia kampeni hiyo, Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga imepokea jumla ya dozi 50,000 za chanjo na hereni 50,000 huku ng'ombe 36,417 wakikusudiwa kuhudumiwa.
Wafugaji wameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuratibu zoezi hilo, wakibainisha kuwa chanjo na hereni zitawasaidia kudhibiti magonjwa, kuboresha biashara ya mifugo na kuongeza tija katika ufugaji.
Kwa upande wake, Daktari wa Mifugo Sila Mbizo anaeleza kuwa magonjwa 13 yanayosumbua mifugo yataweza kudhibitiwa kupitia kampeni hii, huku akisisitiza elimu kwa wafugaji kuendelea kutolewa ili kuhakikisha ufugaji bora na wenye manufaa.
Kampeni hii inalenga kuboresha afya za mifugo, kupunguza magonjwa ya matibabu yenye gharama kubwa kama vile homa ya mapafu, kudhibiti magonjwa ya mlipuko na kulinda afya ya jamii kwa ujumla.








Tunapatikana Kupitia