Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kikosi cha 846 KJ kilichopo Luwa mkoani Rukwa, leo limehitimisha maadhimisho ya kuanzishwa kwake tangu mwaka 1964 kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kutoa matibabu na upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza kwa wananchi.

Katika maadhimisho hayo, wananchi wa kata ya Ntendo inayo jumuisha Vijiji  vya Luwa,Kanondo,Ntendo na Fyengelezya wamepata nafasi ya kupatiwa huduma za afya bure, hatua iliyopokelewa kwa furaha kubwa na wananchi.

Aidha, Luteni Kanali Cuthbert Yohana Mwendi amesema huduma hizo zote zinazotolewa kwa wananchi ni bure, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mshikamano kati ya jeshi na jamii.

Wakizungumza baada ya kupatiwa huduma hiyo, baadhi ya wananchi wameipongeza Serikali na JWTZ kwa kuendelea kuboresha huduma za kijamii, wakisema hatua hiyo inaonyesha mshikamano na ushirikiano wa jeshi na wananchi.


Jeshi la Wananchi wa Tanzania lilianzishwa rasmi tarehe 1 Septemba 1964, likichukua nafasi ya Jeshi la King's African Rifles baada ya uhuru. Tangu wakati huo, limekuwa taasisi yenye mchango mkubwa katika kulinda uhuru, kuimarisha umoja wa kitaifa, na kushiriki kwenye shughuli za kijamii.

Kwa ujumla, JWTZ linaendelea kuwa kielelezo cha uzalendo, ujasiri, na kujitolea kwa ajili ya taifa na watu wake.