Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Rukwa, Hajat Ashraf Maufi, amemuomba mgombea mwenza wa urais, Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi, kufanya maboresho ya barabara ya Bonde la Ziwa Rukwa ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi wa eneo hilo.

Akihutubia wananchi wa Laela, Balozi Dk. Nchimbi amesema serikali ya CCM katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imepiga hatua kubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, ambapo ajira za walimu zimeongezeka kutoka 1,485 hadi 1,960. Aidha, shule za msingi zimeongezeka kutoka 104 hadi 117 na shule za sekondari kutoka 16 hadi 25, hali iliyopanua fursa za kielimu kwa vijana.


Ameongeza kuwa changamoto zote za barabara zitapatiwa ufumbuzi, sambamba na ujenzi wa stendi mpya ya Laela, upanuzi wa huduma za maji safi na salama ili kufikia asilimia 90 ya wananchi, ujenzi wa viwanda vya kusindika chakula na maziwa pamoja na soko la mazao kwa ajili ya kukuza uchumi wa wakulima.

Akizungumza katika mkutano huo, Mchungaji Peter Msigwa, ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ameeleza namna Serikali ya CCM ilivyotekeleza ilani yake ya uchaguzi kwa kipindi cha 2020 hadi 2025. Amesema utekelezaji huo umejidhihirisha kupitia miradi mikubwa ya kitaifa ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, miradi ya maji katika miji 28, na ujenzi wa shule mpya za sekondari ambazo zimepanua fursa za elimu nchini.


Aidha, Msigwa amebainisha kuwa sekta ya afya imepata msukumo mkubwa kwa kujengwa na kuboreshwa hospitali za rufaa, vituo vya afya na zahanati katika maeneo mbalimbali, hatua iliyoinua kiwango cha huduma za afya kwa wananchi. Akisisitiza kuwa CCM ndio chama pekee chenye dira ya maendeleo endelevu ya Taifa, hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kukiamini na kukipa ridhaa ya kuongoza.
Kampeni ya Dk. Nchimbi mkoani Rukwa imeonyesha dhamira ya uongozi thabiti na utekelezaji madhubuti. Kutoka kusema kwa sauti moja kuhusu uchumi sugu hadi kuchukua hatua za uwajibikaji ziwekane wazi. Ujenzi unaoendelea, ufumbuzi wa kero za maji, pamoja na dhamira ya kuwasilisha malalamiko rasmi kwa Rais, ni alama kwamba CCM inaendelea kuimarisha uhusiano na wateule wake.
Ikiwa sehemu ya muendelezo wa ziara kubwa ya maendeleo, tukio hili limeongeza matumaini kwa wananchi wanaosubiri kuona mabadiliko.