Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi linamshikilia Busu Lugwisha (51) mkazi wa kijiji cha Masigo Wilaya ya Mlele Mkoa Katavi kwa tuhuma za kumuua mke wake Regina Thobias (40) baada ya kumpiga na kitu butu kichwani upande wa kisogoni.

Taarifa iliotokewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Katavi Kaster Ngonyani inasema tukio hilo limetokea Februari 19, 2026 majira ya saa 04:00 usiku huko katika kijiji cha Masigo Kata ya llela Tarafa ya Inyonga Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi.

Inaelezwa kuwa uchunguzi wa awali na baada ya mtuhumiwa kuhojiwa umebaini chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi kwani mtuhumiwa amekiri kuhusika na tukio hilo na kueleza kuwa amefanya hivyo kwa kuwa mke wake alimnyima tendo la ndoa.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa chumba cha kuhifadhi maiti kituo cha afya Inyonga "B" kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Mara baada ya taratibu za kipelelezi kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.