Katika juhudi za kukabiliana na vitendo vya kilimo haramu vinavyoathiri usalama na ustawi wa jamii, mamlaka wilayani Butiama mkoani Mara zimeendesha operesheni maalum katika Kijiji cha Mirwa, Kata ya Mirwa, eneo linalopakana na mgodi wa Buhemba. Operesheni hiyo imelenga kubaini na kuchukua hatua dhidi ya shughuli za kilimo cha bangi zilizokuwa zikifanyika kwa siri.

Akiwasili katika eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Thecla Mkuchika alionesha kusikitishwa na uwepo wa kilimo hicho haramu na kutoa onyo kali kwa wanaojihusisha nacho.

Aidha, alielekeza Jeshi la Polisi kuendeleza operesheni kama hizo ili kuwabaini na kuwaondoa kabisa wahusika katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Katika operesheni hiyo, zaidi ya hekari tatu za mashamba ya bangi ziligunduliwa na kuteketezwa kwa moto, pamoja na zaidi ya magunia sita ya bangi iliyokuwa tayari imehifadhiwa kwa ajili ya kusafirishwa na kuingizwa katika matumizi.

Jeshi la Polisi pia lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja aliyekutwa akijihusisha na kilimo hicho katika makazi yake, ambapo ilielezwa kuwa baadhi ya mashamba yalikuwa yamechanganywa na mazao halali kama mahindi na ufuta kwa lengo la kuficha shughuli hiyo haramu.

Baada ya kushuhudia hali hiyo, Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Butiama, Fredi Mmasi alielekeza mashamba yote yaliyobainika kuteketezwa mara moja, huku mtuhumiwa akidai kuwa hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kujihusisha na kilimo hicho na hakutoa majibu ya moja kwa moja alipoulizwa kuhusu ushirikiano na watu wengine.

Akizungumza katika eneo la tukio, kaka wa mtuhumiwa, Chacha Itundura, alisema kuwa mara kadhaa amekuwa akimshauri ndugu yake kuacha kilimo hicho, huku mtuhumiwa akidai kuwa analima kwa mara ya mwisho kabla ya kuacha baada ya mavuno.

Operesheni hiyo ni sehemu ya jitihada za Jeshi la polisi zinazoendelea za kulinda jamii dhidi ya athari za dawa za kulevya na kuhakikisha sheria zinafuatwa.