Jeshi la Polisi Tanzania limewahakikishia wananchi kuendelea kuwa salama huku likisisitiza kuwa linaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa mujibu wa sheria za nchi.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi hilo katika Ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Makao Makuu yaliyopo Dodoma, imeeleza kuwa utekelezaji wa majukumu unaenda sambamba na ushirikiano wa wananchi katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu, hali ambayo imeendelea kuifanya Tanzania kuwa shwari.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, licha ya kuwepo kwa matukio machache ya kihalifu, Jeshi la Polisi limekuwa likiyafanyia kazi na kuwakamata watuhumiwa ambao baadhi yao tayari wamefikishwa mahakamani. Makamanda wa Polisi wa Mikoa wamekuwa wakitoa taarifa hizo mara kwa mara kupitia vyombo vya habari.

Aidha, Jeshi hilo limebaini kuwepo kwa baadhi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuhamasisha wananchi kujihusisha na vitendo vya kihalifu, hususan uhalifu wa kimtandao. Baadhi ya watu hao wamekamatwa huku wengine wakiendelea kutafutwa.

Katika taarifa hiyo, Jeshi la Polisi limekanusha madai yanayosambazwa na watu wanaojitambulisha kwa jina la “TFF” kuwa wanafanya mazoezi porini na kuhusika na matukio ya kijinai. Polisi wamesema taarifa hizo si za kweli na zimelenga kuleta taharuki kwa wananchi.

“Ufuatiliaji unafanyika usiku na mchana. Wananchi waondoe hofu na waendelee na shughuli zao za kiuchumi na kijamii kama kawaida,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Jeshi la Polisi pia limetoa wito kwa wananchi kupuuza jumbe na taarifa zinazotolewa na watu hao, likisisitiza kuwa lengo lao ni kuhamasisha vurugu na kuleta chuki miongoni mwa jamii.

Limeonya kuwa halitasita kumchukulia hatua za kisheria mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo vya kihalifu au kuhamasisha vurugu, kwani ni kinyume na sheria za nchi.

Taarifa hiyo imetolewa chini ya usimamizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Makao Makuu ya Polisi.