Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga Nchini huku Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga ukifikia asilimia 96 ya ukamilishaji wake. Hatua inayoelezwa kuwa ni fursa adhimu kwa sekta binafsi kuwekeza katika huduma za usafiri wa anga na shughuli zinazohusiana na sekta hiyo.

Akizungumza Februari 21, 2026 alipotembelea uwanja wa ndege Sumbawanga Mkoani Rukwa, Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Mwakiposa Kihenzile (MB), ametoa rai kwa wawekezaji na makampuni ya ndege kutumia nafasi hiyo kupanua wigo wa huduma na biashara huku akifafanua kuwa Serikali inaendelea kuboresha viwanja vya ndege Nchini kwa lengo la kuimarisha sekta ya usafiri wa anga na kukuza uchumi wa maeneo husika.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Rukwa na msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Joseph Jemonge, amebainisha kuwa kazi zilizosalia ni hatua za mwisho za ukamilishaji kabla ya uwanja kuanza kutumika rasmi.

Mhe. Kihenzile amesisitiza umuhimu wa kukamilisha kazi hizo kwa wakati ili kuhakikisha huduma zinaanza kutolewa ifikapo Machi 2026, akieleza kuwa kasi ya utekelezaji inapaswa kuendana na matarajio ya Wananchi.

Wananchi pamoja na viongozi wa Mkoa wa Rukwa waliopata fursa ya kufuatilia maendeleo ya mradi huo wameeleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa, wakionesha matumaini makubwa ya kuanza kunufaika na huduma za usafiri wa anga hivi karibuni.

Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Rukwa, kuimarisha biashara na kuongeza mtiririko wa watu na shughuli za maendeleo ndani na nje ya mkoa pamoja na kurahisha mawasiliano na Nchi jirani.