Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga leo Februari 02, 2026 imefanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa mapato ya ndani, ikihusisha sekta za afya na elimu.
Akizungumza mbele ya viongozi na wataalamu mbalimbali, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Utawala, Mhe. Ephraim Konta, amesisitiza mambo yafuatayo baada ya ukaguzi wa miradi hiyo:
Kuongezwa kwa kasi ya umaliziaji wa miradi, sambamba na upatikanaji wa vifaa na malighafi ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.
Wahandisi kuendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya miradi pamoja na mikataba ya mafundi ili kubaini mikataba iliyofikia ukomo na kuifanyia marekebisho panapohitajika.
Amepongeza kukamilika kwa baadhi ya miradi kwa kiwango kikubwa, huku akiwashukuru wananchi kwa kujitoa kwa moyo mmoja katika kufanikisha utekelezaji wa miradi hiyo.
Aidha, Mhe. Konta amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano, hususani katika kujitolea nguvu kazi ili miradi ya elimu na afya ikamilike kwa wakati na jamii ipate huduma bora.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ndugu Chande Juma, amepokea maagizo na maelekezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati, na kuahidi kuwa yatafanyiwa kazi na Menejimenti ya Halmashauri kwa ushirikiano na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji.
Katika ziara hiyo, wajumbe walitembelea miradi mbalimbali ya afya na elimu katika shule za msingi na sekondari ikiwemo Miundombinu ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Mkoa wa Rukwa
Majengo ya madarasa na matundu ya vyoo – Shule ya Msingi Laela “A”,Miundombinu ya Shule ya Msingi Kamnyalile,Madarasa – Shule ya Sekondari Mpui,Zahanati ya Kapewa,Zahanati ya Jangwani.
Ziara hiyo imelenga kuongeza tija ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kwa kubaini changamoto zilizopo na kuzifanyia kazi ili kuwezesha utoaji wa huduma bora kwa jamii ya Sumbawanga.





Tunapatikana Kupitia