Katika juhudi za Serikali kuhakikisha Waheshimiwa Madiwani wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya Utawala bora, Serikali imetoa mafunzo maalum ya Uongozi na Utawala bora kwa Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga na Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, yanayofanyika kwa siku Tatu kuanzia leo Februari 16, 2026 hadi Februari 18, 2026 katika Manispaa ya Sumbawanga.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Charles Makongoro Nyerere, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Mhe. Nyakia Ally Chirukile, amewataka Waheshimiwa Madiwani kuzingatia misingi ya Uongozi bora kwa kuepuka matumizi mabaya ya madaraka huku akisisitiza ushirikiano katika Utendaji Kazi na kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa Madiwani kuwa wabunifu katika kutatua changamoto za jamii, kushiriki kikamilifu katika utekelezaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo, pamoja na kuepuka migongano ya kimaslahi binafsi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Bi. Pendo Mangali, amesema Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na Waheshimiwa Madiwani ili kuhakikisha Wananchi wanapata huduma bora na maendeleo endelevu kupitia usimamizi mzuri wa shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma kwa umma.
Nao Waheshimiwa Madiwani walioshiriki mafunzo hayo wameishukuru Serikali kwa kuwapatia mafunzo hayo muhimu, wakieleza kuwa yameongeza uelewa, weledi na uwezo wao wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi, huku wakiahidi kuzingatia misingi ya Uongozi bora kwa manufaa ya Wananchi na maendeleo ya maeneo yao.













Tunapatikana Kupitia