Mexico imewatuma wanajeshi 10,000 mitaani kutuliza mapigano yaliyosababishwa na mauaji ya mlanguzi mkubwa wa dawa za kulevya nchini humo ambaye amesababisha vifo vya watu wengi.

Nemesio "El Mencho" Oseguera, kiongozi wa Genge la Jalisco New Generation (CJNG), alijeruhiwa Jumapili katika makabiliano ya risasi na wanajeshi katika mji wa Tapalpa, katika jimbo la Jalisco, na akafariki alipokuwa akisafirishwa kwa ndege hadi Jiji la Mexico.

Habari za kifo chake zilisababisha vurugu, huku wafuasi wake wakifunga barabara katika majimbo 20 na kuchoma magari na majengo. Waziri wa Usalama Omar Garcia Harfuch alisema kiasi ya maafisa 25 wa Jeshi la Ulinzi wa Taifa waliuawa katika mapigano yaliyozuka. Harfuch aliongeza kuwa mlinzi mmoja wa gereza, afisa wa ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali na washukiwa 30 wa kundi la uhalifu aliloongoza Oseguera pia waliuawa.

Karibu mahabusu 23 wakitoroka wakati gereza lao liliposhambuliwa kwa risasi nyingi na "makundi ya wahalifu," kulingana na waziri wa usalama wa jimbo la Jalisco. Wakazi waliojawa na hofu walijificha majumbani na watalii wakajificha katika hoteli zao kutokana na machafuko ya wafuasi wa genge hilo.