Urusi iliivamia kikamilifu Ukraine Februari, 24, 2022, kitendo kilichoibua vita vikubwa kabisa ambavyo havijashuhudiwa barani Ulaya tangu vile vya Pili vya Dunia. Ukraine inafanya kumbukumbu ya miaka minne.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen na Rais wa Baraza hilo António Costa wanatarajiwa mjini Kiev Jumanne huku Ukraine ikifanya kumbukumbu ya miaka minne ya uvamizi kamili wa Urusi.

Vita hivyo vimesababisha uharibifu mkubwa nchini Ukraine. Miji yote mashariki na kusini mwa Ukraine, miongoni mwao Bakhmut, Toretsk na Vovchansk, imeharibiwa na mapigano. Shirika la Afya Duniani WHO limethibitisha zaidi ya mashambulizi 2,800 kwenye vituo vya afya tangu mwaka wa 2022, huku mashambulizi ya Urusi kwenye miundombinu ya nishati yakiathiri mifumo ya kupasha joto majumbani na huduma za umeme kwa mamilioni ya wakaazi.

 Karibu thuluthi moja ya Ukraine imeharibiwa na mabomu ya kutegwa ardhini au mabomu ambayo hayajalipuka, kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na uratibu na utekelezaji wa miradi ya kukabiliana na kitisho cha mabomu ya kutegwa ardhini UNMAS.

Gharama ya jumla ya ujenzi mpya nchini Ukraine inakadiriwa kuwa karibu dola bilioni 588 katika muongo mmoja ujao, kwa mujibu wa Benki ya Dunia.