Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Deus Clement Sangu amewasili mkoani Rukwa kwa ziara ya kikazi inayolenga kuimarisha ajira, kukuza ujuzi na kuendeleza ustawi wa vijana pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii.

Akizungumza mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Sangu ameeleza kuwa ziara hiyo inalenga kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili vijana, wajasiriamali na wafanyakazi, sambamba na kuhamasisha matumizi bora ya fursa zinazotolewa kupitia Sera, Sheria na mipango mbalimbali ya Serikali.

Mheshimiwa Sangu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kwela mkoani Rukwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya ajira na uwekezaji, ikiwemo kuimarisha mafunzo ya stadi za kazi, kukuza ubunifu na teknolojia, pamoja na kuimarisha mahusiano mazuri kati ya waajiri na wafanyakazi ili kuongeza tija na ushindani katika soko la ajira.

Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Waziri Sangu anatarajiwa kufanya mikutano ya hadhara na vikao vya majadiliano na vijana, wajasiriamali, waajiri na vyama vya wafanyakazi, kwa lengo la kupokea maoni yao na kutoa maelekezo ya namna bora ya kunufaika na programu za ajira, mafunzo ya ufundi na mikopo ya uwezeshaji.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa imewahimiza wadau wote kujitokeza kushiriki kikamilifu katika vikao na mikutano itakayofanyika wakati wa ziara hiyo, ili kwa pamoja kuendelea kuujenga Mkoa wa Rukwa ulio na fursa nyingi za kiuchumi, mshikamano wa kijamii na maendeleo jumuishi.