Waziri wa Vijana Mh. Joel Nanauka, amewataka vijana wa Mkoa wa Sjhinyanga wasiwe watazamaji katika shughuli za kiuchumi bali wachangamkie fursa ya kumiliki uchumi kupitia fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali, ikiwemo shilingi bilioni 200 zilizotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya kuwawezesha kupitia majukwaa yao ya vijana.

 Waziri Nanauka ameyasema hayo, wakati akizindua Jukwaa la Vijana la Mkoa wa Shinyanga, na kudai kuwa serikali imejipambanua kuhakikisha kwamba vijana wanapata nafasi ya kujiendeleza kiuchumi kupitia raslimali zinazopatikana hapa nchini ikiwemo uchimbaji wa madini, viwanda, kilimo na ufugaji. 

 Nao baadhi ya vijana walioshiriki katika uzinduzi wa Jukwaa hilo, wamesema shauku yao ni kuona nchi inakuwa na mabadiliko makubwa ya maendeleo, baada ya serikali kuona kuwa vijana wakiwezeshwa wanaweza kufanya mambo makubwa kulingana na ndoto zao.

 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, amesema licha ya serikali kutenga bajeti ya kuyawezesha makundi ya Vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, kupitia fedha za asilimia 10 ya mapato ya ndani, shilingi bilioni 200 za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zinaenda kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya vijana kwa kufungua fursa mbalimbali wanazozitarajia.