Jeshi
la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia mvuvi mmoja, Ndaishimiye Gerald Joseph
(45), mkazi wa Kisiwa cha Zilagula, kwa tuhuma za kumuua mvuvi mwenzake, James
Jastine Lameck (45), kufuatia wivu wa kimapenzi.
Tukio hilo la kikatili lilitokea alfajiri ya tarehe 19 Februari, 2026, majira
ya saa 10:30 katika Kisiwa cha Zilagula, Kijiji cha Itabagumba, Wilaya ya
Sengerema.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP
Wilbroad Mutafungwa, Februari 20, 2026, mtuhumiwa anadaiwa kumpiga marehemu
ngumi sehemu mbalimbali za mwili wake na kisha kumnyonga shingoni kwa kutumia
mikono hadi kifo kilipomfika.
“Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi,
baada ya aliyekuwa mke wa mtuhumiwa, Neema Mathias Lwasa, kutengana naye
Februari 05, 2026 na kuanza uhusiano mpya na marehemu, ambapo walikuwa wakiishi
pamoja katika makazi ya marehemu ndipo mtuhumiwa alipopata wivu na kwenda
kutenda tukio hilo la kikatili”, imeeleza taarifa ya polisi.
Mwili wa marehemu James Jastine umeshafanyiwa uchunguzi wa kitabibu na
kukabidhiwa kwa familia yake kwa ajili ya taratibu za mazishi. Jeshi la Polisi
limesisitiza kuwa linaendelea kumhoji mtuhumiwa na mara baada ya upelelezi
kukamilika, atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za mauaji.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limetoa onyo kali kwa
wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi. Wamewasihi wananchi
kutumia njia sahihi za kutatua migogoro ya kifamilia na kijamii, ikiwemo
kuwashirikisha ndugu, viongozi wa dini, au kufuata taratibu za kisheria kupitia
vyombo husika badala ya kutumia vurugu.
Tunapatikana Kupitia