Jamii imetakiwa kuimarisha na kuenzi ushirikiano kupitia majadiliano yenye tija, hatua itakayosaidia kujenga Taifa lenye ustawi na maendeleo endelevu.

Wito huo umetolewa na Mbunge wa Kwela ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi, Deus Sangu, wakati wa ziara yake katika Kata ya Laela na Kata ya Kasanzama, zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Februari 24, 2026.Ziara hiyo imelenga kuhamasisha ushirikiano, mshikamano na kuimarisha mahusiano miongoni mwa jamii

Akiwa katika mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo mkubwa wa kilovoti 400 (400kV) wa gridi ya taifa unaotekelezwa kutoka Tunduma hadi Sumbawanga, Waziri Sangu aliielekeza kampuni ya Sinohydro Corporation Limited kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa umakini na ubora unaotakiwa ili wananchi wa Sumbawanga wapate huduma ya umeme wa uhakika.

Waziri Sangu alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati ili wananchi wanufaike na kuboresha maisha yao.

Katika hatua nyingine, Waziri Sangu alieleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo pamoja na mifumo ya usimamizi wa rasilimali watu, huku akipongeza juhudi zinazofanywa na mkandarasi katika kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa kuzingatia viwango vinavyokidhi matakwa ya kisheria na kitaaluma.

Aidha, alimtaka mkandarasi huyo kuzingatia kwa umakini suala la Usalama na Afya Mahali pa Kazi pamoja na kuendelea kuchangia katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (National Social Security Fund (NSSF)) kwa kulipa michango ya wafanyakazi kwa mujibu wa sheria.

Akitoa taarifa mbele ya Waziri, Mwakilishi wa kampuni ya Sinohydro ambaye pia ni Meneja wa Rasilimali Watu na Mahusiano, Ndugu Maghembe Noni, aliahidi kuwa kampuni itaendelea kushirikiana na Serikali huku ikizingatia sheria, kanuni na taratibu za kazi.

Waziri Sangu yupo katika ziara ya kikazi katika Jimbo la Kwela.