Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Mhe. Nyakia Ally Chirukile amepiga marufuku uuzaji holela wa viwanja unaofanywa na baadhi ya Wananchi bila kufuata Sheria, Taratibu, Kanuni, Miongozo na Maelekezo ya uuzaji wa maeneo, hali inayochochea migogoro ya ardhi katika Jamii.

Mhe. Chirukile ametoa marufuku hiyo leo Februari 18, 2026, wakati alipotembelea eneo lenye mgogoro katika Mtaa wa Shengetela Kata ya Lwiche Wilayani Sumbawanga. Eneo lililoripotiwa kuwa na mgogoro kati ya Evarist Chambula na Evance Misonge, ambapo chanzo cha mgogoro huo ni mauziano ya eneo la jirani na Evance Misonge yasiyo halali yaliyofanywa na Evarist Chambula kwa mtu mwingine, huku kwa mujibu wa ramani eneo hilo likitambulika kuwa ni barabara.

Mhe. Chirukile amesema Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya Wananchi wanaojihusisha na uuzaji wa viwanja au maeneo kinyume cha Sheria, ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha kwa mujibu wa Sheria za Nchi.

Aidha, Mhe. Chirukile amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia Sheria na kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unalindwa wakati wote, huku akiwataka wananchi kufuata taratibu sahihi za umiliki na uuzaji wa ardhi ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.