Kiongozi ni mtu mwenye mamlaka au ushawishi wa kuwaongoza watu wengine kwa kuwaelekeza, kusimamia, kuwahamasisha na kuwajibika katika kufikia malengo fulani ya pamoja.Sifa za kiongozi bora katika taasisi ni msingi wa mafanikio, mshikamano na maendeleo endelevu ya taasisi husika. Kiongozi bora si yule mwenye cheo tu, bali ni yule anayehakikisha taasisi inasonga mbele huku akilinda na kuzingatia maslahi ya wafanyakazi.

Zifuatazo ni sifa muhimu za kiongozi bora:

1. Uadilifu na Uwajibikaji

Kiongozi bora huwa mwadilifu, mkweli na anawajibika kwa maamuzi yake. Hafanyi upendeleo wala matumizi mabaya ya rasilimali za taasisi.

2. Kuhakikisha Maslahi ya Wafanyakazi

  • Anasimamia haki zao (mishahara, posho, likizo, mafao n.k.)

  • Anasikiliza malalamiko na changamoto zao

  • Anaunda mazingira salama na rafiki ya kazi

  • Anahamasisha mafunzo na maendeleo ya kitaaluma

Kiongozi bora hutambua kuwa wafanyakazi ndiyo nguvu kazi ya taasisi.

3. Uwezo wa Kusikiliza na Kuwashirikisha Wengine

Hushirikisha wafanyakazi katika maamuzi muhimu. Hatoi maamuzi ya juu juu bila kushauriana. Hujenga utamaduni wa maoni na ushirikiano.

4. Maono (Vision) na Mwelekeo

Kiongozi bora huwa na dira ya wazi ya taasisi – anajua taasisi inatoka wapi na inakwenda wapi. Huweka mikakati ya kufikia malengo kwa ufanisi.

5. Uwezo wa Kufanya Maamuzi Sahihi

Hufanya maamuzi kwa kuzingatia sheria, kanuni na maslahi mapana ya taasisi badala ya maslahi binafsi.

6. Haki na Usawa

Huwatendea wafanyakazi wote kwa usawa bila ubaguzi wa jinsia, dini, kabila au ukaribu wa kibinafsi.

7. Uwezo wa Kutatua Migogoro

Kiongozi bora hutatua migogoro kwa hekima na busara bila kupendelea upande wowote.

8. Uwazi katika Uendeshaji

Hutoa taarifa muhimu kwa wafanyakazi kuhusu maendeleo ya taasisi, bajeti, mipango na changamoto.

9. Kuwa Mfano Bora

Hutangulia kwa vitendo – nidhamu, uwajibikaji, kuheshimu muda na kuheshimu wengine.

10. Kuhamasisha na Kuthamini Wafanyakazi

Hutoa pongezi pale panapostahili, hutambua juhudi za wafanyakazi na kuwapa motisha ya kufanya kazi kwa bidii zaidi na sio kuwavunja moyo wafanyakazi.

Mwisho.