Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa magonjwa ya mlipuko nchini yakiwemo mafua makali ya Influenza, UVIKO-19, Homa ya Dengue na Kipindupindu.
Akitoa taarifa hiyo, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace E. Magembe, amesema Wizara imeendelea kufuatilia mwenendo wa magonjwa ya mlipuko, ambapo hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko la wagonjwa wa mafua makali ya Influenza na UVIKO-19.
Amesema magonjwa hayo huenezwa kupitia majimaji yanayotoka kwenye mfumo wa njia ya hewa wa mgonjwa mwenye maambukizi wakati wa kukohoa, kupiga chafya au kuzungumza. Pia yanaweza kuenezwa kwa kugusa mazingira yaliyochafuliwa na majimaji hayo.
Dalili zake ni pamoja na homa kali, kikohozi, maumivu ya kichwa na mwili, mafua, kuwashwa koo na uchovu.
Kwa mujibu wa takwimu za ufuatiliaji, kila mwaka kati ya mwezi Novemba hadi Aprili, kunakuwa na ongezeko la magonjwa hayo hapa nchini na duniani. Kutokana na hali hiyo, wananchi wanashauriwa kuchukua tahadhari zifuatazo:
-
Kufunika pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya.
-
Kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono.
-
Kuepuka misongamano isiyo ya lazima.
-
Kuvaa barakoa unapokuwa na dalili, unapokuwa karibu na mtu mwenye dalili au ukiwa kwenye maeneo yenye msongamano.
-
Kuzingatia usafi binafsi na wa mazingira.
-
Kuwahi kituo cha kutolea huduma za afya kupata matibabu stahiki na kuepuka kujitibu au kutumia antibiotiki bila ushauri wa wataalam wa afya.
Aidha, Wizara imeonya kuhusu ongezeko la Homa ya Dengue katika baadhi ya maeneo ya nchi kufuatia mvua za masika zinazopelekea kuongezeka kwa mazalia ya mbu.
Homa ya Dengue huenezwa na mbu aina ya Aedes, ambaye ni mweusi mwenye madoa meupe na hupendelea kuuma nyakati za asubuhi, mchana na jioni. Dalili zake ni pamoja na homa kali, maumivu ya kichwa na viungo, maumivu nyuma ya macho na uchovu, na mara nyingi huchanganywa na dalili za malaria.
Wananchi wanashauriwa:
-
Kutokomeza mazalia ya mbu ikiwemo makopo yaliyotupwa hovyo, matairi ya magari, vifuu na kufukia madimbwi ya maji kutuama.
-
Kujikinga kwa kuvaa nguo ndefu, kutumia dawa za kufukuza mbu na kuweka nyavu madirishani.
-
Kuwahi kituo cha afya kupata huduma stahiki.
Kuhusu ugonjwa wa Kipindupindu, Wizara imesema nchi imekuwa katika mlipuko ulioathiri mikoa yote isipokuwa Kilimanjaro na Njombe. Hata hivyo, katika kipindi cha takriban mwezi mmoja uliopita, hakuna mgonjwa mpya aliyeripotiwa.
Serikali imetambua mchango wa sekta mbalimbali, taasisi za dini, viongozi wa jamii, wanahabari, sekta binafsi, wadau chini ya usimamizi wa Shirika la Afya Duniani pamoja na jamii kwa ujumla katika kudhibiti mlipuko huo.
Pamoja na mafanikio hayo, bado kuna hatari ya kuibuka kwa maambukizi mapya kutokana na mvua zinazoendelea na uwepo wa maambukizi katika nchi jirani.
Wananchi wanakumbushwa kuendelea kuchukua tahadhari zifuatazo:
-
Kuchemsha maji ya kunywa au kutibu kwa dawa maalum kama Aquatab au Waterguard na kuyatunza vizuri.
-
Kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni kabla ya kula, baada ya kutoka chooni, baada ya kumhudumia mtoto aliyejisaidia na kabla ya kumnyonyesha mtoto.
-
Kuosha matunda kwa maji safi kabla ya kula na kuepuka kula vyakula vya baridi au vilivyoandaliwa katika mazingira yasiyo safi.
-
Kujenga vyoo bora, kuvitumia na kuviweka katika hali ya usafi nyakati zote.
-
Kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya maji kwa kujisaidia, kutupa taka au kutiririsha maji taka.
-
Kutunza mazingira na kuepuka kutupa taka ovyo.
Serikali imeeleza kuwa itaendelea kufuatilia kwa karibu magonjwa yote ya mlipuko na kutoa taarifa mara kwa mara endapo kutakuwa na mabadiliko ya mwenendo wa maambukizi au itakapohitajika kuchukua hatua zaidi.


Tunapatikana Kupitia