Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, ameipongeza
Mahakama ya Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha haki,
ustawi wa jamii na maendeleo ya Taifa kwa ujumla, akieleza kuwa Mahakama
ni mhimili muhimu unaolinda misingi ya usawa na utawala wa sheria.
Mheshimiwa
Makongoro ametoa pongezi hizo alipokuwa mgeni rasmi katika maadhimisho
ya Siku ya Sheria Nchini kwa Mkoa wa Rukwa, yaliyofanyika katika viwanja
vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala ya Sumbawanga. Maadhimisho hayo
yaliwakutanisha wadau mbalimbali wa haki na wananchi, yakilenga
kutafakari mchango wa Mahakama katika maendeleo ya Taifa.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Mheshimiwa Makongoro amesema Mahakama ina jukumu la
kipekee la kutoa haki kwa wananchi bila upendeleo, akisisitiza kuwa
utoaji wa haki kwa weledi na kwa wakati ni msingi wa kudumisha amani na
mshikamano katika jamii.
Aidha, Mheshimiwa Makongoro ametoa rai
kwa Mahakama kuendelea kusogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi kwa
kupanua wigo wa utoaji wa huduma, ikiwemo ujenzi wa vituo vya Mahakama
kwa kushirikiana na wananchi. Amebainisha kuwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa
wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia shughuli za maendeleo ya
Taifa, hivyo wanastahili huduma za haki zilizo karibu nao.
Mheshimiwa
Makongoro pia ameipongeza Mahakama Kanda ya Sumbawanga kwa utendaji
kazi wake mzuri, akisema umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa
maendeleo ya kijamii na kiuchumi mkoani hapa.
Mahakama ya
Tanzania huadhimisha Siku ya Sheria Nchini kila Mwaka, ambapo siku hiyo
huashiria mwanzo rasmi wa Mwaka wa shughuli za Mahakama Tanzania. Ni
siku muhimu ya kutathmini utendaji wa Mahakama na kuweka mwelekeo wa
utoaji haki kwa Mwaka mzima.
Maadhimisho ya Siku ya Sheria
Tanzania kwa Mwaka 2026 yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Mchango wa
Mahakama katika ustawi na maendeleo ya Taifa”, kauli mbiu inayolenga
kuhimiza uwajibikaji, ufanisi na ushirikishwaji wa wananchi katika mfumo
wa utoaji haki nchini.
Tunapatikana Kupitia