Rais wa Marekani Donald Trump amefuta chapisho lake kwenye mitandao ya kijamii lililokuwa likimfananisha rais wa zamani Barack Obama na mkewe Michelle kama nyani.

Chapisho hilo limekosolewa vikali na wanasiasa kutoka upande wa Republican na Democrats na kutajwa kuwa lenye kukera na la ubaguzi wa rangi.

Baada ya ukosoaji huo, Ikulu ya White House ilisema kuwa mfanyakazi mmoja alichapisha video hiyo kimakosa. Hata hivyo, Trump amesema hataomba msamaha akidai kuwa hakufanya kosa lolote.

Video hiyo, yenye muda wa takriban dakika moja, ilihusisha madai ya udanganyifu kwenye uchaguzi wa mwaka 2020, lakini mwishoni ilionyesha sura za familia ya Obama zilizopachikwa juu ya vichwa vya sokwe huku wimbo wa “The Lion Sleeps Tonight” ukipigwa.