Wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga Wilayani Sumbawanga Mkoani Rukwa, wameanza kunufaika na mpango wa bima ya afya kwa wote baada ya Mkuu wa Wilaya Mhe. Nyakia Ally Chirukile kuwakabidhi bima baadhi ya Wananchi katika Kata ya Sumbawanga, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Hatua ambayo ni miongoni mwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati akilihutubia Bunge, ambapo alieleza dhamira ya Serikali kuhakikisha wananchi wote wanapata fursa ya kujiunga na bima ya afya ndani ya siku 100 za mwanzo za Uongozi wake.

Akizungumza katika zoezi hilo, Mhe. Chirukile amesema mpango huo unalenga kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa wananchi na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya bila vikwazo vya kifedha. Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi wote kwa usawa.

Aidha, amewahimiza wananchi waliopokea bima hiyo kuitunza na kuitumia kwa usahihi ili waweze kunufaika kikamilifu na huduma zinazotolewa katika vituo vya afya.

Kwa upande wao, wananchi walionufaika wameishukuru Serikali kwa kutimiza ahadi yake, wakieleza kuwa bima hiyo itasaidia kupunguza gharama za matibabu na kuongeza ustawi wa maisha yao kwa ujumla.