Maelfu ya waombolezaji wamekusanyika mjini Islamabad leo kwa ibada ya mazishi ya watu 31 waliouawa jana katika shambulizi la kujitoa mhanga kwenye msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Ibada ya mazishi kwa baadhi ya waathiriwa ilifanyika katika eneo la wazi karibu na msikiti huo chini ya ulinzi mkali.

Waziri wa habari Attaullah Tarar amesema serikali inawafuatilia waliohusika katika shambulizi hilo na kuongeza kuwa baadhi ya waathiriwa bado wako mahututi hospitalini wanapoendelea kupokea matibabu.

Katika ujumbe kupitia mtandao wa X, waziri wa ulinzi Khawaja Asif, amesema mshambuliaji huyo alikuwa na historia ya kusafiri hadi Afghanistan, na ameilaumu India kwa kuhusika katika shambulizi hilo bila ya kutoa ushahidi wowote.

Kwa upande wake, ofisi ya mambo ya nje ya India imelaani shambulizi hilo na kukanusha madai kwamba ilihusika kivyovyote vile.