Tanzania chini ya uongozi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania maendeleo ya jamii na haki za kijamii yameimarika na kuwa kati ya vipaumbele vya Ajenda ya Kitaifa inayojumuishwa katika mfumo wa kisera na kisheria wa nchi ikiwa ni pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na utekelezaji wake ukinyumbulishwa katika Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2050 ambayo pia huakisi utekelezaji wa Ajenda za kikanda na kimataifa kama Maendeleo Endelevu 2030.

Hayo yamesemwa katika Kikao cha 64 cha Tume ya Maendeleo ya Jamii (CSocD64) na Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania kwenye Kikao hicho Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon A. Mpanju, wakati wa Kikao hicho kinachofanyika jijini New York nchini Marekani kuanzia tarehe 2 Februari 2026 na kinatarajiwa kuhitimishwa tarehe 10 Februari 2026.

 

Wakili Mpanju amesema amesema Tanzania inaendeleza sera zenye kuratibiwa vyema katika ukuaji wa uchumi na Ulinzi wa Jamii, maendeleo ya rasilimali watu, na upatikanaji sawa wa huduma za msingi. Juhudi hizo zinaimarishwa na sera za kisekta zinazoendana na ulinzi wa jamii, usawa wa kijinsia, maendeleo ya vijana, elimu, afya, na ulinzi wa makundi maalum hususan Wanawake,Wazee,Watoto na watu wenye ulemavu sambamba na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu namba (SDGs) 1, 5, 8, 10, na 16. 

 Wakili Mpanju ameeleza kuwa katika ulinzi wa kijamii Tanzania imeongeza wigo kwa kiasi kikubwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambapo katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 zaidi ya wanufaika milioni 1.26 wamefikiwa wakiwakilisha kaya zote maskini zilizotambuliwa, ambapo walengwa walipokea ruzuku za fedha. Hatua hizi zimeimarisha usalama wa kipato cha kaya, kuboresha upatikanaji wa huduma za elimu na afya, na kuongeza uhimilivu dhidi ya mishtuko ya kiuchumi na changamoto za tabianchi.

Aidha, ameongeza kuwa Tanzania imepiga hatua katika usawa wa kijinsia, uwezeshaji vijana na ushirikishwaji wa jamii ambapo Ushiriki wa wanawake katika uongozi na maamuzi umeendelea kuongezeka katika mihimili na ngazi mbalimbali za kiutawala za serikali mathalani idadi ya wabunge kwenye Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania imeongezeka na kufikia 40.5%. Suala hili la ongezeko la idadi ya wanawake imechagizwa na uwepo wa mipango na bajeti zenye mlengo wa jinsia ambapo kupitia mpango wa 10% wa Mikopo ya Mapato ya Ndani ya kila Halmashauri, mikopo isiyo na riba inaendelea kutolewa kwa wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu wanaojishughulisha na shughuli ndogo za kiuchumi.