Watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wameuawa katika majibizano ya risasi na Polisi katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi, mkoani Simiyu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe, amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo, Februari 8, 2026, majira ya saa nane usiku, katika mtaa wa NMB, Kata ya Malambo, Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Kamanda Swebe amesema polisi walipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna watu wanavunja milango ya jengo la Simiyu Money Services, linalotumika kutoa huduma za kifedha.
Amesema kikosi maalumu cha kupambana na uhalifu kilifika eneo hilo, na watuhumiwa waliokuwa wanatekeleza uhalifu walipobaini kuwa wanafuatiliwa, walianza kufyatua risasi, na kufuatia hali hiyo polisi walilazimika kujibu mapigo kwa usalama.
Watuhumiwa hao walifariki dunia wakati wakipelekwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Aidha, askari walifanikiwa kupata silaha moja aina ya AK-47 iliyokuwa ikitumiwa na watuhumiwa hao wa ujambazi pamoja na risasi nane ndani ya magazini.

Tunapatikana Kupitia