Rais Samia Suluhu Hassan amesema kukamilika kwa Soko Kuu jipya la Kariakoo lililopo mkoani Dar es Salaam kunaleta mageuzi makubwa ya kibiashara, baada ya maboresho yanayowawezesha wafanyabiashara wengi kupata nafasi ya kufanya biashara zao kwa utaratibu mzuri na wenye tija.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa soko hilo leo Februari 8, 2026, akiwa mgeni rasmi, Rais Samia amesema anahitaji kusikia usawa bila upendeleo na ukiritimba wakati wa ugawaji wa maeneo ya biashara, hususan kwa wale waliokuwepo awali na kuathirika na ajali ya moto.
Rais Samia ameongeza kuwa haitakuwa busara kwa viongozi wa Serikali Mkoa wa Dar es Salaam na wenye mamlaka katika soko hilo kujipa kipaumbele kwenye fursa za kugawa maeneo ya biashara, na kuwataka wasimamie kwa haki, hasa kwa wafanyabiashara waliolengwa kufanya biashara ndani ya soko hilo.
Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa mamlaka za mapato zisimamie ukusanyaji wa kodi kwa weledi, huku akisisitiza uwazi katika taarifa za mapato na matumizi ya fedha za soko hilo la kimataifa.
Soko jipya la Kariakoo limejengewa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 28, likiboresha miundombinu na kutoa nafasi kubwa zaidi kwa wafanyabiashara kufanya biashara ndani ya soko.
Ujenzi huo umefanywa kufuatia moto ulioharibu soko la awali, ili kurejesha shughuli za biashara na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara kwa wafanyabiashara waliokuwa wakilitumia soko la zamani.


Tunapatikana Kupitia