Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mwigulu Lameck
Nchemba, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule ya Amali ya Mkoa wa
Rukwa inayojengwa katika Kata ya Majengo, wilayani Nkasi, leo Machi 9,
2026.
Shule hiyo ya amali inayotoa mafunzo ya ufundi inajengwa
kwa gharama ya shilingi bilioni 1.6 na katika awamu ya kwanza
inatarajiwa kuwa na jumla ya majengo 19, yakiwemo jengo la utawala,
madarasa, maabara, karakana za mafunzo, bwalo la wanafunzi pamoja na
vyoo.
Kwa mujibu wa taarifa ya mradi, hadi sasa ujenzi wa
madarasa nane pamoja na jengo la utawala umekamilika na miundombinu hiyo
tayari imeanza kutumika. Aidha, ujenzi wa jengo la TEHAMA na maktaba,
nyumba ya mtumishi pamoja na vyoo vya wavulana na wasichana pia
umekamilika na majengo hayo yanaendelea kutoa huduma.
Ujenzi wa
miundombinu mingine unaendelea katika hatua mbalimbali, ikiwemo karakana
ya uashi iliyo katika hatua ya ufungaji wa mfumo wa umeme, karakana ya
ufundi magari na mitambo iliyo katika hatua ya uwekaji wa sakafu na
ufungaji wa umeme, pamoja na mabweni manne ambapo matatu yako katika
hatua ya uwekaji wa dari na moja katika hatua ya uwekaji wa sakafu na
dari.
Mradi huo unatarajiwa kuongeza fursa za mafunzo ya ufundi
stadi kwa vijana wa Mkoa wa Rukwa na maeneo jirani, hatua
itakayowawezesha kujiajiri na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi
ya mkoa na Taifa kwa ujumla.
Waziri Mkuu yuko mkoani Rukwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu iliyoanza Machi 8, 2026.

.jpeg)

.jpeg)
Tunapatikana Kupitia