WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Jumatatu, Machi 9, 2026 ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Amali ya Mkoa wa Rukwa iliyopo katika Kata ya Majengo, Namanyere, Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.
Mradi huo unatekelezwa kupitia Programu ya Kuboresha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) kwa gharama ya shilingi bilioni 1.6 na unalenga kuboresha elimu ya ufundi stadi kwa kuwaandaa wanafunzi kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuchangia maendeleo ya kiuchumi ya Taifa.
Mradi huo ulianza kutekelezwa Desemba 20, 2024 na ulitarajiwa kukamilika Machi 30, 2025, ambapo hadi sasa jumla ya shilingi bilioni 1.5 zimetumika katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya mradi, hadi sasa ujenzi wa madarasa nane pamoja na jengo la utawala umekamilika na miundombinu hiyo tayari inatumika. Pia ujenzi wa jengo la TEHAMA na maktaba, nyumba ya mtumishi pamoja na vyoo vya wavulana na wasichana umekamilika na miundombinu hiyo imeanza kutumika.
Halikadhalika, ujenzi wa miundombinu mingine unaendelea katika hatua mbalimbali ikiwemo karakana ya uashi ambayo ipo katika hatua ya ufungaji wa mfumo wa umeme, karakana ya ufundi magari na mitambo iliyo katika hatua ya sakafu na ufungaji wa umeme pamoja na mabweni manne ambapo matatu yako katika hatua ya dari na moja katika hatua ya sakafu na dari.





Tunapatikana Kupitia