Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa kupitia Mtandao wa Polisi Wanawake, wakiongozwa na mlezi wa mtandao huo ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Shadrack Masija, wamewafikia na kuwagusa watu wenye uhitaji maalum katika mtaa wa Vuta, Manispaa ya Sumbawanga kwa kuwapatia msaada wa mahitaji mbalimbali ikiwemo viti mwendo kwa watoto wenye ulemavu.

Akizungumza 19 Machi 2026 wakati wakikabidhi msaada huo, SACP Masija alihimiza jamii kuendelea kudumisha upendo, mshikamano na umoja, huku akisisitiza umuhimu wa kuwajali watu wenye uhitaji maalum katika jamii zinazowazunguka. 

Aidha, alitoa wito kwa wananchi na familia zenye watu wenye ulemavu kuacha tabia ya kuwaficha, kuwanyanyapaa au kuwanyanyasa, na badala yake wawapatie haki zao za msingi kama binadamu wengine.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa wa Rukwa, Mrakibu wa Polisi Faustina Mwakapangala, alisema kuwa mtandao huo utaendelea kushirikiana na jamii katika kusaidia makundi yenye uhitaji maalum ili kujenga jamii yenye usawa na utu.

Familia za walengwa wa msaada huo zililishukuru Jeshi la Polisi pamoja na Mtandao wa Polisi Wanawake kwa kuwagusa na kuwatia moyo, huku wananchi wa eneo hilo wakiahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi katika kudumisha amani, usalama na kushiriki kikamilifu katika juhudi za kutokomeza uhalifu.