Wananchi wa Mkoa wa Songwe, hususan wa Wilaya ya Momba katika Mji wa Tunduma, wametakiwa kuwa watulivu, kupuuza uvumi usio na ukweli na kuendelea na shughuli zao za maendeleo bila hofu, kufuatia taharuki iliyosababishwa na taarifa za imani za kishirikina zinazosambaa katika maeneo hayo.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mheshimiwa Jabir Makame, alipofanya mikutano katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Tunduma tarehe 03 Aprili 2026 katika Mtaa wa Kilimanjaro, Kisimani na Majengo (eneo la Soko la Mazao Tunduma), akiongozana na Kamati ya Usalama ya Mkoa. 

Mh. Makame, amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyotokana na wananchi kujichukulia sheria mkononi, huku akiwahakikishia wananchi kuwa vyombo vya dola vinaendelea kufuatilia kwa karibu hali hiyo na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahusika.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga, alisema kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limefanya mikutano hiyo kwa wananchi kwa lengo la kutoa elimu na kutuliza taharuki iliyojitokeza, baada ya kuenea kwa uvumi wa kuwepo kwa watu wanaodaiwa kugusa wenzao na kusababisha kupotea kwa sehemu za siri hali iliyopelekea baadhi ya wananchi kujeruhiwa na mtu mmoja kupoteza maisha.

Kamanda Senga, amekemea vikali vitendo vya wananchi kuwashambulia watu kwa tuhuma zisizo na uthibitisho na kusisitiza kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria, huku ameeleza kuwa Jeshi la Polisi halitavumilia vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, na yeyote atakayebainika kuhusika na vurugu au kusababisha taharuki atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Mwisho. Kamanda Senga aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati, pamoja na kuepuka kusambaza au kuamini taarifa zisizo na uthibitisho ambazo zinaweza kuhatarisha amani na usalama wa jamii.