Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa limethibitisha kukamatwa kwa watu 25 kufuatia tukio la mauaji ya Henry Shubati Myuwanga, mwalimu wa Shule ya Msingi Wema iliyopo mkoani Songwe.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Tanzania, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Aprili 4, 2026 katika Kijiji cha Kilyamatundu, Wilaya ya Sumbawanga.
Inaelezwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa kibiashara uliotokana na kutokubaliana bei ya sabuni kati ya marehemu na kijana mmoja muuza duka kijijini hapo. Baada ya kutokea kwa sintofahamu, kijana huyo alidai kupoteza fahamu na kuibua tuhuma kuwa mwalimu huyo alihusika na imani za kishirikina.
Taarifa zinaeleza kuwa kelele za kijana huyo ziliwavutia wananchi waliojitokeza kwa wingi na kuanza kumshambulia mwalimu huyo kwa kumpiga mawe kabla ya kuchoma moto mwili wake, hali iliyosababisha kifo chake papo hapo.
Polisi wamesema msako mkali unaendelea ili kuwabaini na kuwakamata wote waliohusika katika tukio hilo, huku wakionya vikali vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi.
Aidha, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kupuuza na kutoa taarifa sahihi kuhusu uvumi unaozua taharuki, hususan madai yanayohusisha wizi wa viungo vya mwili wa binadamu kwa imani za kishirikina


Tunapatikana Kupitia