Maafisa kilimo wa Kata ya Nkandasi, Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa wamezindua kanuni kumi (10) mpya za kilimo zenye lengo la kuongeza tija kwa wakulima na kuboresha hali ya maisha kupitia uzalishaji wenye manufaa zaidi.

 Uzinduzi huo umefanyika katika Kijiji cha Kasu na kuhudhuriwa na wakulima pamoja na wananchi mbalimbali waliopata nafasi ya kuelimishwa kuhusu mbinu bora za kilimo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Diwani wa Kata ya Nkandasi, Richard Mpemba, amewahimiza wakulima kuzingatia kanuni na maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa kilimo ili kuongeza uzalishaji na kuhakikisha wanapata mazao yenye ubora na faida zaidi sokoni.

 Afisa Kilimo wa Wilaya ya Nkasi, Adam Dege, amesema serikali inaendelea kutoa elimu na ushauri kwa wakulima ili kuwajengea uwezo wa kulima kisasa na kwa tija na kueleza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha wakulima wanatumia mbegu bora, mbinu sahihi za uhifadhi wa udongo pamoja na teknolojia rahisi zitakazoongeza uzalishaji na kuinua kipato cha kaya nyingi vijijini.