Na fedrick Mbaruku -Rukwa
Askofu wa Kanisa la PHAMT Jimbo la Sumbawanga, Ezekia Mwahalende, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanatoa malezi bora kwa watoto kwa kuwajenga katika misingi imara ya imani na maadili, akisema hatua hiyo itasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto katika jamii ya sasa ikiwemo vitendo vya ukatili.
Askofu Mwahalende ameyasema hayo leo Juni 17,2026 katika kanisa la PENTECOSTE HOLINESS ASSOCIATION MISSION TANZANI (PHAMT) JIMBO LA SUMBAWANGA ambapo amesema familia ndiyo nguzo kuu ya malezi ya mtoto, hivyo wazazi wanapaswa kutenga muda wa kutosha kuwaelekeza watoto wao katika njia sahihi za maisha, kuwafundisha hofu ya Mungu na kuwajengea tabia ya kuheshimu utu na haki za wengine ili wawe raia wema wa baadaye.
Aidha, amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya wazazi, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya vitendo vya ukatili, matumizi mabaya ya mitandao na mmomonyoko wa maadili, huku akihimiza jamii kuendelea kuwekeza katika malezi yanayozingatia upendo, maadili na imani.
Kwa upande wake Leonard Mwanjisi Mkurugenzi wa Idara ya watoto PHAMT, Jimbo la Sumbawanga amesema walimu wana nafasi kubwa katika jamii juu ya kupambana na vitendo vya ukatili huku akibainisha kuwa ni wajibu wao kushirikiana na Serikali, wazazi,walezi na wadau wengine katika kutatua migogoro, kutoa elimu kuhusu madhara ya ukatili, na kulinda haki za watoto na wanawake.
"Kila mwalimu anapaswa kuwa mstari wa mbele kukemea ukatili wa aina yoyote na kuhamasisha vijana kuishi kwa amani, heshima na uwajibikaji katika jamii,"amesema mwanjisi.
Mussa Ambindwile Mwambije ni Mchungaji wa Kantalamba Bethania Center na Katibu wa kanisa la PHAMT jimbo la sumbawanga ameeleza namna ushirika wa makanisa hayo unavyosaidia kuleta mabadiliko chanya katika jamii. Alisema kwamba, pamoja na mchango wao wa kiroho, makanisa yana jukumu pia la kijamii, kama vile kusaidia watu wasiojiweza na kuhamasisha amani. Hivyo, ni muhimu kwa kila mmoja wetu kushirikiana ili kufanikisha malengo hayo, ndani ya jamii.

Tunapatikana Kupitia