Waganga wa tiba asili na tiba mbadala wametakiwa kuacha vitendo vya uganga vinavyohatarisha maisha ya watu na kuepuka ramli chonganishi zinazoweza kuvuruga amani katika jamii.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Mhe. Nyakia Ally Chirukile, wakati akifungua kikao cha waganga wa tiba asili na tiba mbadala kilichofanyika Agosti 25, 2025 kwa lengo la kujadili maendeleo na kudumisha tunu ya Taifa ya amani na utulivu.


Mhe. Chirukile ameeleza kuwa katika kipindi cha uchaguzi kumekuwepo na matukio yanayochochewa na imani za kishirikina ambapo baadhi ya waganga wamekua wakihusika kwa kufanya ramli chonganishi.

Aidha, amewasisitiza waganga hao kuwa mabalozi wa amani, pamoja na kuhimiza wananchi kushiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025 kwa kusikiliza sera za wagombea na kuchagua viongozi bora.

Pamoja na wajibu huo, waganga wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti, ikizingatiwa kuwa tiba mbadala hutegemea mizizi, magome, majani na matunda kutoka katika miti na mimea mbalimbali.


Mratibu wa tiba asili na tiba mbadala wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Musa Mbalamwezi, amesema waganga wanapaswa kushirikiana na Serikali kwa kuhakikisha wagonjwa wanahimizwa kufika vituo vya kutolea huduma za afya kwa wakati wanapougua ili kuepuka vifo vinavyotokana na ukosefu wa huduma stahiki.

Naye Mwenyekiti wa Waganga wa tiba asili na tiba mbadala Mkoa wa Rukwa, Michael Jackson, anaeleza kuwa waganga wa jadi wapo bega kwa bega na Serikali katika kuhakikisha jamii inakuwa salama na inapata tiba kupitia njia asilia, huku wakiahidi kutoa elimu kwa wananchi kuhusu wajibu wao katika kipindi cha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika oktoba 29, 2025.