Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema ahadi zote zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kuwa zitatekelezwa ndani ya siku 100 za utawala wake zimetekelezwa.
Kauli hiyo imetolewa leo, Februari 8, 2026, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Soko Kuu jipya la Kariakoo, Dar es Salaam, uzinduzi uliofanywa na Rais Samia aliyekuwa mgeni rasmi.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa Rais Samia aliahidi mengi wakati wa kampeni, na miongoni mwa ahadi zilizotekelezwa ni kutoa ajira za walimu 7,000 pamoja na ajira zaidi ya 5,000 katika sekta ya afya.
Aidha, Dkt. Nchemba amesema kuwa nchi inasonga mbele huku akiwakumbusha Watanzania kuchangamkia fursa za kibiashara, ikiwa ni pamoja na ile inayotolewa kupitia soko jipya la Kariakoo.
Soko hilo jipya limejengewa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 28, likiboresha miundombinu na kutoa nafasi kubwa kwa wafanyabiashara kufanya biashara ndani ya soko.
Ujenzi huo umefanywa kufuatia moto ulioharibu soko la zamani, na ulilenga kurejesha shughuli za biashara pamoja na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara kwa wafanyabiashara waliokuwa wakilitumia soko la awali.

Tunapatikana Kupitia