Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Mhe. Nyakia Ally Chirukile amesisitiza umuhimu kwa jamii kuzingatia matumizi sahihi ya chakula chenye makundi yote ya lishe ili kuhakikisha afya bora na kuepuka tatizo la udumavu katika jamii.

Mhe. Chirukile amesema ni muhimu kwa Wananchi kutumia mazao wanayolima kwa kuzingatia mlo kamili, badala ya kujikita katika aina moja ya chakula, ili kuimarisha afya za watoto katika ngazi ya kaya na jamii kwa ujumla.

Wito huo ameutoa leo Februari 20, 2026, wakati akizungumza katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Robo ya Pili 2025/2026.

Aidha, amesisitiza kuwa lishe bora ni msingi wa maendeleo ya jamii hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha anatumia vyakula vyenye makundi yote ya chakula ili kujenga jamii yenye afya na nguvu kazi imara.