1. Usuli
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo (81) jana Alhamis, Februari 19, 2026 aliitwa katika nyumba ya Milele ya Bwana akiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, jijini Dar es Salaam. Hii ni kwa mujibu wa Taarifa iliyosainiwa kwa pamoja na Mhashamu Thaddeus S. Ruwai'chi OFMCap, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, na Mheshimiwa Padri Vicent Mpwaji, Kansela. Kifo hiki kimetokea baada ya kurudishwa toka India kwani itakumbukwa Desemba 24, 2025, Mhashamu Baba Askofu Ruwa'ichi alitoa Taarifa kuwa Mwadhama Polycalp Kadinali Pengo alikuwa anapelekwa nchini India kupata matibabu.
Miaka kadhaa iliyopita, nilipata fursa adimu na adhimu ya kumtembelea Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo. Ilikuwaje? Mwanayanga mwenzangu, marehemu Prof. Benno Ndulu, aliyekuwa Gavana wa Sita wa Benki Kuu ya Tanzania, siku moja alinipigia simu saa 8 usiku akiwa yuko Seychelles. Nikiwa nimelala fofofo, nikawa naskia kwa mbali simu inaita mfululizo. Nikawa naipotezea. Ilipozidi kuita, nikaamka kutaka kuweka "silent mode". Nikaona "missed calls" 10 na namba ya nje ya nchi. Nikaamua kuipokea. Kumbe alikuwa ni Prof Ndulu ambaye alinitaka radhi kwa kupiga simu usiku wa maa'nan na kisha akaniomba kesho yake asubuhi niende kumwona Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ili kumsaidia jambo lake moja lililokuwa likimtatiza sana.
Kesho yake asubuhi na mapema nikaenda kwa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ambaye alinipokea kwa ukarimu ingawa alionesha dhahir kuwa na huzuni. Nafurahi kuwa nilifanikiwa kutatua kilichokuwa kikimsibu na kumrudishia furaha yake ya kawaida.
Kisha nikaitumia fursa hiyo kumhoji kwa kirefu kuhusu historia ya maisha yake. Nilimhoji kwelikweli. Ndiyo maana Atikali hii ina mambo mengi ya kipekee ambayo Bongolanders wengi hawayajui kuhusu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Siku hiyo nilifurahi sana kwa kupata baraka ya kukutana na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo. Nilijiona mwenye bahati kubwa hasa nilipokumbuka kuwa nilipokuwa altar boy, kanisa la Mtakatifu Petro nikisoma Oysterbay Primary School mimi na altar boys wenzangu tulibahatika kuwa tukishika kisahani (paten) wakati Mwadhama Laurean Kadinali Rugambwa alipokuwa akimlisha mkate Rais Julius Kambarage Nyerere ambaye kila saa 12 asubuhi alikuwa akija kusali kanisani hapo na waamini wengine. Kabla na baada ya kuanza misa, altar boys tulikuwa tukiongea na Mwadhama Laurean Kadinali Rugambwa ambaye alikuwa na utaratibu wa kutupatia pipi. Tulimpenda sana. Kwa upande mwingine, tulikuwa tukishangaa alivyokuwa akija kanisani akiwa ndani ya Volkswagen ambayo ilikuwa ikiendeshwa na Sista. Tulikuwa tukishangaa kwa jinsi alivyokuwa mtu wa miraba minne kuweza kuenea kwenye gari hiyo! Mmoja kati ya hao altar boys wenzangu ni Bw Melchiades Domino Rutayebesibwa ambaye sasa ni Meneja wa Huduma za Kibenki, Benki Kuu, Tawi la Ntwara.
Siku niliyoenda kuonana na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, nilipiga nae picha ya ukumbusho ambayo nimeiambatisha kwenye Atikali hii. Nilijiona mwenye bahati ya kipekee maishani kwa kuweza kuwa karibu na Makardinali wawili wa Kitanzania, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa, aliyekuwa Mwafrika wa kwanza kuwa Kardinali.
Wakati tukiomboleza msiba huu mkubwa, nimeandaa Atikali hii maalum kwa heshima ya Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ambayo inayavinjari maisha yake toka kuzaliwa kwake.
1. Kuzaliwa
Mwadhama Polycalp Kadinali Pengo alizaliwa adhuhuri ya Jumamosi, Agosti 5, 1944 katika Parokia ya Mwazye, dayosisi ya Sumbawanga, Tanganyika (Tanzania). Baba yake aliitwa Joseph Pengo, ambaye alitokea Nothern Rhodesia (Zambia) na mama yake aliitwa Rosaria Nzyungu. Wawili hawa walikutana kanisani baada ya Bw Pengo kuwa amehamia Tanganyika, wakapendana kisha wakaoana.
Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliwajalia Bw & Bi Joseph Pengo kupata watoto tisa. Polycarp alikuwa mtoto wa sita kati ya watoto hao tisa. Wawili kati ya hao tisa walifariki wakiwa wadogo sana kabla ya Polycarp hajazaliwa hivyo hakuwaona.
Mzaliwa wa kwanza, aliyezaliwa mwaka 1933, alikuwa mwanamke. Huyu alikuwa ndiye dada yake mkubwa. Kwakuwa Polycarp alikuwa na wito wa kuwa padri na alikuwa akiueleza mara kwa mara huku akifurahishwa na mavazi na madevu ya White Fathers, dada huyu mkubwa aliweka "nadhiri" kuwa lazma atahakikisha mdogo wake anatimiza tamanio lake, aslan abadan.
Dada huyu, akiwa bado binti mdogo, alienda kwa Masista waliompatia nafasi ya kujifunza ualimu hatimaye akatunukiwa cheti cha Ualimu. Akajiapiza kuwa hatakuja kuolewa hadi mdogo wake afanikiwe, hivyo alitumia mapato yake ya ualimu kulipia ada ya shule na mahitaji mengine. Hakutaka kuona fedha inakuwa kikwazo kwa mdogo wake.
2. Masomo
Polycarp, ambaye ni Mfipa, alisoma shule ya msingi pale parokiani kwao na akiwa mdogo kabisa akaingia kwenye mfumo wa kujiandaa kuwa Padri. Mhashamu Askofu Charles Msakila aliyekuwa parokia ya Ipito, ambako kulikuwa na a preparatory seminary, alimlea kiroho kuanzia darasa la 4 alipomchukua yeye na wenzie wachache wakakaa kwa mwaka mmoja kisha wakaenda seminari ndogo ya Karema. Huko Karema walikaa kwa miaka miwili kisha mwaka 1959 wakaingia seminari ya Kaengesa walikosoma hadi Kidato cha nne, mwaka 1964. Sifa za uongozi alianza kuzionesha mapema na hapo seminari ya Kaengesa alikuwa Kiranja Mkuu Msaidizi na mwanafunzi mwenye akili sana darasani.
Miongoni mwa Bongolanderz maarufu waliokuja kusoma seminari ya Kaengesa baadaye (notable alumni) ni Mhe Mizengo Pinda, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Mhe Arcado Ntagazwa, aliyewahi kuwa Waziri, Mhe Deus Sangu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Gabriel Simon Mnyele, Wakili Msomi aliyewahi kuwa DC Uyui, Prof MKB Wambali & Prof Juan Mwaikusa, waliowahi kuwa Wahadhiri wa Kitivo cha Sheria UDSM, Richard Wambali aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Benki Kuu, Tawi la Dodoma, Justine Jumbe Shofeli Rumanyika, ambaye anafanya utume wake kama Meneja wa Mipango-Mkakati, Benki Kuu, Tawi la Dar es Salaam, na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, Mhashamu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga.
Mwaka 1965, Polycarp alijiunga na St Paul Major Seminary, Kipalapala, Tabora iliyoanzishwa Februari 4, 1925 na White Fathers. Alisomea Falsafa na akahitimu mwaka 1967.
Miongoni mwa watu maarufu waliokuja kusoma seminari hii baadaye ni Prof Adelardus Kilangi, aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na Jean Baptiste Frezal Charbonnier, ambaye baadaye aliandika historia ya kuwa Askofu wa kwanza wa Equatorial Guinea.
Kuweza kufika seminari ya Kipalapala, ambako ada haikuhitajika, ilimaanisha ndoto ya Polycarp ilikuwa inatimia hivyo dada yake akatoa sadaka maalum na kumshukuru Mungu kwa kumjalia mdogo wake kutumiza azma yake, kisha akaolewa umri ukiwa umeenda.
Mwaka 1968 hadi 1971, Polycarp alisoma Theolojia hapohapo Seminari Kuu ya Kipalapala.
3. Ushemasi
Baada ya mwaka wa Tatu wa Theolojia, Polycarp akapata Ushemasi mwezi Desemba 1970.
4. Upadri
Polycarp alipewa daraja la Upadri Juni 20, 1971. Alipewa daraja hilo na Mhashamu Askofu Charles Msakila jimboni Sumbawanga.
Mhashamu Askofu Msakila alikuwa amebuni utaratibu mujarab kuwa Mashemasi wote wapate Dominica ya Upadrisho kwenye Parokia zao ili kuhamasisha vijana wengine kupenda Upadri.
Kwa Sumbawanga walikuwa Mashemasi wanne; Polycarp, Godfrey Mwanisawa, Alphonce Kayanda na Paul Chanzi.
Polycarp na Godfrey Mwanisawa, ambaye alikuwa binadamu yake, walitokea parokia ya Mwazye.
Siku hiyo, ilikuwa ni furaha kubwa kwenye parokia hizo na wananchi walifurahi sana ambapo walikula na kusaza na Sute ilinyweka sana.
Kuanzia mwaka 1971 hadi 1973, Mheshimiwa Padri Pengo alikuwa Katibu wa Askofu wa Jimbo la Sumbawanga.
Awali alikuwa na hofu sana baada ya Mhashamu Askofu Msakila kumtaka awe Katibu wake kwani alijiona bado mdogo na aliamini hiyo ni kazi ya watu wenye umri mkubwa kwa kumuangalia mtangulizi wake wa kutoka Uholanzi, Padri Jacobs, ambaye alikuwa mtu mzima. Hata hivyo, alijipa moyo na kutimiza wajibu wake vizuri sana.

5. Masomo Roma
Mwaka 1973, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) liliandaa mpango kabambe wa kuwapeleka Mapadri vijana hodari kwenda kusoma Roma. Hivyo, ikampendeza Mwenyezi Mungu kuwa Mheshimiwa Padri Pengo (28) naye awe mmoja wa Mapadri hao waliochaguliwa kwenda Roma mwaka 1973 katika chuo kikuu cha kipapa la Lateran, Kitivo cha Taalimungu, Maadili cha Alphonsianum ili kujifunza Maadili ya Kanisa.
Ilijitokeza changamoto kubwa kwani Mhashamu Askofu Msakila alipatwa tatizo la moyo na alikuwa akipelekwa Ujerumani kwa matibabu hivyo akapata ugumu kumwachia Mheshimiwa Padri Pengo lakini mwishowe hakuwa na jinsi.
Mheshimiwa Padri Pengo alisoma na wenzie na wakahitimu shahada ya Uzamivu katika masomo ya Theolojia ya Maadili mwaka 1977.
6. Kurejea Nchini
Baada ya kufuzu masomo yake, Mheshimwa Padri Pengo alirejea nchini mwanzoni mwa mwaka 1977 na akaelekezwa na TEC kwenda kuwa Mwalimu na Mlezi katika Seminari Kuu ya Kipalapala. Alianza kufundisha wale waliokuwa mwaka wa kwanza wa Theolojia. Miongoni mwao alikuwepo Mhashamu Thaddeus Ruwa'ichi, ambaye sasa ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, na Almachius Vicent Rweyengeza, ambaye sasa ni Mwashamu Askofu.
Mheshimiwa Padri Pengo alikaa Seminari Kuu ya Kipalapala kwa muda wa miezi tisa.
7. Ugambera Seminari ya Segerea
Mwaka 1978, Mheshimiwa Padri Pengo alipata heshima kubwa alipoteuliwa na TEC kuwa Gambera wa kwanza katika Seminari Kuu ya Segerea ambayo ilianza rasmi mwaka 1979. Alipata mstuko na woga kwani alijiona bado mdogo na kwakweli kwa umri wake kuwa Gambera wa kwanza ilikuwa ni jukumu zito lakini akasali sana na kuomba Mungu amwongoze.
Mheshimiwa Padri Pengo alikaa Seminari Kuu ya Segerea kwa miaka sita akiwa ameifanyia mengi na aliweka misingi imara.
8. Uaskofu
Novemba 11, 1983, Baba Mtakatifu Yohane Paul wa II alimteua Mheshimiwa Padri Pengo kuwa Askofu wa Jimbo la Nachingwea.
Januari 6, 1984, Mheshimiwa Padri Pengo aliwekwa Wakfu katika Daraja Takatifu la Uaskofu katika Basilika ya Mtakatifu Petro huko mjini Vatican, Roma. Yeye alikuwa Mtanzania wa Pili kupewa Uaskofu na Papa huko Roma, akitanguliwa na Mwashamu Askofu Charles Msakila. Wakati yeye alipewa na Papa Yohane Paul wa II, Mwashamu Askofu Msakila alipewa na Papa Yohane wa XXIII Desemba 28, 1958.
Mhashamu Askofu Pengo alihamishiwa Nachingwea baada ya Mmarekani "Msalvatori", Mhashamu Askofu Anord, kustaafu kwavile umri ulikuwa umeenda. Wakati huo, Mhashamu Askofu Pengo alikuwa kijana sana.
Oktoba 17, 1986, Mhashamu Askofu Pengo alitangazwa kuwa Askofu wa Jimbo jipya la Tunduru -Masasi na alisimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo hilo Februari 12, 1987.
Kuwa Askofu wa kwanza kwenye jimbo jipya tena lililoko pembezoni mwa nchi ukiwa kijana mdogo ilikuwa ni shughuli pevu. Pevu sana. Lakini Mhashamu Askofu Pengo alilitekeleza jukumu hilo kwa ustadi wa hali ya juu ambapo alianzisha parokia kadhaa kama vile Hulia, Muhuwesi (ambako alijenga seminari ndogo) na akajenga makao ya Askofu Tunduru.
9. Uaskofu Mkuu Mwandamizi Dsm
Mwaka 1990, ilionekana umri wa Mwadhama Laurean Kadinali Rugambwa ulikuwa umeenda hivyo ikabidi atafutwe Askofu mwingine ili amsaidie na wakati huohuo aanze kujifunza majukumu.
Hivyo, Januari 22, 1990, Papa Yohane Paul II akamtangaza Mhashamu Askofu Pengo kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam mwenye haki ya kurithi jimbo hilo.
Kama kawaida yake, Mhashamu Askofu Pengo alipata hofu. Aliwaona waamini wa jiji la Dar es Salaam ni "wajuaji" na wamezoea miaka yote kuongozwa na Kardinali lakini yeye alikuwa ni Askofu tu tena kijana mdogo aliyetokea Usweken Tunduru, lakini akapiga moyo konde!
Baada ya Mwadhama Laurean Kadinali Rugambwa kustaafu, Mhashamu Askofu Pengo alisimikwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Julai 22, 1992.
Licha ya hofu yake ya hapo mwanzo, kama ilivyokuwa kote kwingine alikopitia, alilimudu vyema jukumu hilo jipya.
10. Ujio wa Papa
Papa Yohane Paul II aliwasili nchini Septemba 2, 1990 kwa ziara rasmi ya kidini. Hili lilikuwa tukio la kihistoria kwani ilikuwa mara ya kwanza kwa Papa kuzuru nchini. Mhashamu Askofu Pengo, aliyekuwa Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ndiye aliyetoa hotuba pale Kanisa la Mtakatifu Petro, Oysterbay. Hii ilikuwa ni heshima kubwa sana kwake.

11. Ukardinali
Februari 22, 1998, Papa Yohane Paulo II alimchagua Mhashamu Askofu Pengo kuwa mmoja wa Makardinali wapya. Hii ilikuwa ni wiki chache tu baada ya Mwadhama Laurean Kadinali Rugambwa kufariki hapo Desemba 8, 1997 na Tanzania kuandika historia ya kuwa nchi ya kwanza kutoa tena Kardinali katika muda mfupi toka Kardinali mwingine afariki. Mwandishi nguli, Stanley Kamana, akaandika kwenye gazeti la "East African" :
"Pope John Paul II's soft spot for Tanzania led to the swift appointment of Cardinal Pengo after the death of the first ever African Cardinal, Laurean Cardinal Rugambwa. Pope John Paul II was a great friend of the country".
Mhashamu Askofu Pengo akasimikwa rasmi hadhi hiyo ya Ukardinali April 26, 1998, siku ambayo Tanzania ilikuwa ikiadhimisha miaka 34 ya Muungano.
12. Wafipa Wasimamia Mazishi ya Mwalimu JK Nyerere Butiama
Mazishi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, yaliyofanyika Jumamosi, Oktoba 23, 1999, yalisimamiwa na Wafipa watatu.
Mwenyekiti wa Kamati ya mazishi kitaifa, alikuwa Mhe Paul Kimiti. Aliyesoma Misa ya mazishi ni Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na aliyesimamia Jeshi alikuwa Kanali Kisango. Hawa wote watatu walikuwa wafipa.
13. Mwadhama Polycalp Kadinali Pengo Aandaa "Dinner" kwaajili ya Rais Mkapa
Mwaka 2005, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliandaa dinner maalum kwenye ukumbi wa kanisa la Mtakatifu Joseph kwaajili ya kumshukuru Mungu kwa kumuwezesha Rais Benjamin Mkapa kumaliza salama ngwe yake ya Urais (1995-2005).
Dinner hiyo ilifanyika siku mbili baada ya Mhe Mkapa kukabidhi madaraka. Waliohudhuria ni pamoja na Mhashamu Baba Askofu Methodius Kilaini, Mama Anna Mkapa, Mhe Nico Mkapa na mkewe Folster na Bw William Erio na mkewe Janet. Bw. Erio ni mpwa wa marehemu Rais Mkapa na pia ni Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa PPF, NSSF na FCC.
14. Urais wa Baraza la Maaskofu
Mwaka 2007, Mwadhama Polycalp Kadinali Pengo alichaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Afrika na Madagascar. Urais huo uligota 2013.

15. Kumchagua Papa Benedict XVI
Papa huchaguliwa na Makardinali ambao umri wao ni chini ya miaka 80.
Katika historia ya Taifa letu, Makardinali watatu wamewahi kushiriki kumchagua Papa.
Mwadhama Laurean Kadinali Rugambwa, ambaye Machi 28, 1960 aliweka historia ya kuwa Kardinali wa kwanza Afrika, ndiye alikuwa wa kwanza kumchagua Papa. Alishiriki kwenye kuutoa moshi mweupe mwaka 1964 alipochaguliwa Papa Paul VI. Pia, alishiriki kumchagua Papa Yohane Paul I hapo Agosti 26, 1978 na Papa Yohane Paul II hapo Oktoba 16, 1978.
Mwadhama Polycalp Kadinali Pengo alishiriki kumchagua Papa Benedict XVI hapo April 19, 2005.
Mwadhama Protace Kadinali Rugambwa alishiriki kumchagua Papa Leo XIV Mei 8, 2025.
16. Mwadhama Polycalp Kardinali Pengo Aibariki Nyumba ya Rais Mkapa
Mei 10, 2011, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alimtembelea Rais Mstaafu Ben Mkapa nyumbani kwake Oysterbay. Akiwa nyumbani hapo, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alipata Lunch na Rais Mkapa, Mama Anna Mkapa, Mhe Nico na mkewe Folster , Bw William Erio na mkewe Bi Janet, familia ya Benard Mkapa na ya ukoo wa Maro.
Kisha, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akaibariki nyumba hiyo chumba kwa chumba na akawapa wote zawadi za rozari zilizokuwa zimebarikiwa na Papa Benedict XVI.
17. Kumchagua Papa Francis
Kama ilivyoelezwa hapo juu, Papa huchaguliwa na Makardinali ambao umri wao ni chini ya miaka 80.
Mwaka 2005, Mwadhama Polycalp Kadinali Pengo hakuwa amefikisha miaka 80 bali alikuwa na miaka 61 hivyo alishiriki kumchagua Papa Francis hapo Machi 13, 2013.
18. Jubilee ya Miaka 25 ya Uaskofu Mkuu wa Jimbo
Jumamosi, Julai 22, 2017, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alisheherekea Miaka 25 ya kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

19. Kujiuzulu
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliongoza Jimbo Kuu la Dar es Salaam toka Julai 22, 1992 hadi Agosti 15, 2019 alipojiuzuru baada ya kutimiza miaka 75 kwa mujibu wa Kanuni. Kanuni ya 40(1) ya Kanisa inaeleza:
"A diocesan Bishop who has completed his seventy-fifth year of age is requested to offer his resignation from office to the Supreme Pontiff, who, taking all the circumstances into account, will make provision accordingly"
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alikuwa ameomba kujiuzulu na ombi lake lilikubaliwa na Papa Francis.
Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Padri Dr Charles Kitima, Katibu wa TEC, Papa alielekeza Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amwachie Mwashamu Askofu Mkuu, Thadei Ruwa'ichi, ambaye alikuwa amemteua Juni 21, 2018 kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam akitokea Mwanza alikokuwa Askofu Mkuu wa Jimbo hilo.
20. Jubilee ya Miaka 50 ya Upadri
Juni 20, 2021, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alitimiza miaka 50 ya daraja la Upadri. Sherehe ya kukata na shoka ikafanyika kanisa la Msimbazi ambapo waamini toka dayosisi mbalimbali walihudhuria na pia Maaskofu na Mapadri toka sehemu mbalimbali nchini.
20.1 Rais Samia Ampa Cheti
Kwenye Jubilee hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan alimpa Cheti maalum "Certificate of Recognition" Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kwa kutambua mchango wake mkubwa kwa Taifa letu. Rais aliwakilishwa na Makamu wa Rais, Dkt Isidory Mpango.
20.2 Ruwa'ichi Ampa Tshs 25M
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Askofu Ruwa'ichi, alimkabidhi Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo cheki ya Benki ya Mkombozi yenye thamani ya Tshs 25,000,000/= kwa niaba ya Jimbo kama shukrani yao kwa utume wake jimboni hapo.
21. Magonjwa
Afya ya Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ilianza kudorora miaka mingi iliyopita.
Alipatwa na tatizo la mgongo na kupelekea awe anatembea kwa msaada ya mkongojo. Mwaka 2014, akihubiri katika ibada ya misa maalum iliyoandaliwa na UWAKA (Umoja wa Wanaume Katoliki) kituo cha kiroho Mbagala, Mwadhama alisema:
"Kwa muda sasa nimekuwa sionekani kwa kuumwa. Najua wengi wanashangaa kumuona Askofu wao akitembea kwa mkongojo. Nawashukuru wote kwa kuniombea, sasa nina nafuu".
Januari 1, 2016, Rais John Magufuli na mkewe, Mama Janeth Magufuli, walimtembelea kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alikokuwa amelezwa. Baadaye aliruhusiwa kutoka hospitalini.
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alilazimikq kufanyiwa operesheni tatu za uti wa Mgongo. Operesheni mbili za kwanza alifanyia India.
Alipofanyiwa operesheni ya pili nchini India, alikosa fahamu kwa siku kadhaa akiwa ICU hadi Mheshimiwa Padri Vicent Mpwaji na Sista Stela waliomsindikiza wakaingiwa na hofu na kutuma ujumbe huku nyumbani kuwa hali sio hali na kuwaomba waamini waongeze sala za kumwombea.
Alipozinduka, yule daktari aliyemfanyia operesheni alistuka na kushangaa sana na hakujua dawa gani imemsaidia kwani alijua kuwa "Huyu mgonjwa ni wa leo au wa kesho"!
Aliporejea nchini, akashindwa kusimama wima ikabidi baadaye akafanyiwe ya tatu New York, Marekani mwezi Mei 2017.
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliwahi kufafanua kuwa tofauti na wengi wanavyoamini, shida yake kubwa miaka ya hivi karibuni sio mgongo bali moyo. Alisimulia kuwa kabla ya kufanyiwa operesheni ya mgongo New York, madaktari walipoupima moyo wake walibaini una mushkeri sana na wakatafakari sana kama moyo wake ungeweza kuhimili operesheni hiyo. Akafafanua kuwa ndio maana alilazimika kwenda mara mbili kwani mara ya kwanza ilikuwa ni kwaajili ya wao kumfanyia uchunguzi wa kina na kufanya tafakuri jadidi. Akapewa madawa ya moyo ya kumsaidia hususan afikapo Tanzania.
Alipoenda kufanyiwa operesheni ya mgongo, madaktari walimwambia operesheni yake ingekuwa ya muda mrefu, masaa 8 au 9. Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akawaambia yeye anawaachia kila kitu, Mungu akipenda ataamka lakini kama siku zake zimefika yeye yuko tayari kwa hilo na akasema itakuwa jukumu la madaktari kuwaeleza Watanzania kilichotokea.
Operesheni ikachukua masaa 12 na madaktari wakawa na hofu sana na moyo lakini akapata ahueni ya ajabu.

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alisimulia pia kuwa aliwahi kupata shida kubwa ya moyo alipomsindikiza Mhashamu Askofu Titus Joseph Mdoe alipohamishiwa Mtwara ambapo alishindwa kabisa hata kuhudhuria ibada. Januari 26, 2014, Mhashamu Mdoe alieleza kwenye misa Takatifu iliyofanyika Kigango cha Nzasa, Temboni jimboni humo kuwa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo hali yake ilikuwa si nzuri na kuwaomba waamini wamwombee.
Ikabidi Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo arudi na alazwe Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambako Prof Mohammed Janabi aliokoa uhai wake.
22. Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo Aenda India kwa Matibabu
Desemba 24, 2025, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Juda Thaddeus Ruwai'chi, alieleza kuwa afya ya Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu la DaresSalaam, licha ya matibabu aliyokuwa akipatiwa hapa nchini, imedhoofu hivyo alikuwa akipelekwa nchi India kwa matibabu zaidi.
23. Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo Alijiandalia Kaburi
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alijiandalia kaburi lake ambamo alipenda aje kuzikwa atakapotangulia mbele za Haki. Akaandika akifa azikwe Pugu.
Kaburi hilo tayari liliishachimbwa.
Waamini walipokuwa wakimuuliza kuwa haoni kuwa kwa kufanya hivyo alikuwa anajichulia, jibu lake siku zote lilikuwa ni kuwa mwisho wa binadamu ni kifo, iwe kaburi limechimbwa au la!
Agosti 13, 2019, aliandika:
"Kuna kaburi langu pale Pugu. Naomba liheshimiwe. Nawasihi viongozi wote wa Kanisa, Waamini na wengine wote kuwa nikifa nizikwe kwenye kaburi langu Pugu".
Awali, maneno haya aliyaeleza kwenye sherehe yake ya kutimiza miaka 75 Agosti 5, 2019.
Mimi ninavyohisi ni kuwa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alichagua eneo hilo la Pugu kwavile, kwa mawazo yangu, ni eneo la kihistoria. Hapa ndipo chimbuko la Kanisa nchini kwani ndipo dini ya Katoliki ilipohubiriwa kwa mara ya kwanza mwaka 1888. Hapo ndio mahali ambapo Wafia-Dini watatu ambao walikuwa Wamishenari toka Ujerumani (Mtawa Martha na Mabruda Petrus na Benedict) waliuawa na wafuasi wa Chifu Abushiri.
24. Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo Hakupenda Michezo
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo hakupenda mchezo wa aina yoyote. Agosti 13, 2019, aliandika :
"Mimi sio mpenzi wa Michezo hata kidogo; kiasi kwamba kule seminari ndogo Kaengesa nililazimika kucheza mpira wa miguu kwa lazima, ambao pia nilikuwa siuwezi, kwakuwa michezo ilikuwa ni lazma".
25. Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo Awamwagia Wachagga Maua Yao
Januari 9, 2025, jimbo Katoliki Moshi lilikuwa na Upadrisho wa Mashemasi 18, ambapo Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alihudhuria.
Mwisho wa misa, Askofu Mkuu wa Jimbo la Moshi, Mhashamu Askofu Ludovick Joseph Minde, alimpa fursa kutoa neno.
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alitumia fursa hiyo kuwamwagia maua yao Wachagga kwa kusema kuwa Wachaga sio wezi kama inavyodaiwa. Alisema yeye akiwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam alifanya nao kazi kwa karibu na walimsaidia sana kujenga Kanisa, kufanikisha azma yake ya kanisa kujitegemea na maendeleo makubwa yalionekana kutokana na wao kushika nafasi nyingi za uongozi. Alimalizia kwa kusema kama ni tabia ya udokozi basi ni ya mtu na si Wachagga na kuwa wezi wapo mmojammjoja toka kwenye makabila mbalimbali mf Wasukuma, Wafipa na wengine.
26. Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo Aongoza Misa ya Kumbukizi ya Miaka 5 ya kifo cha Rais Mkapa
Asubuhi, Julai 23, 2025, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliongoza misa ya kumbukizi ya miaka 5 ya kifo cha marehemu Rais Mkapa iliyofanyika Lupaso.
Mchana, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alipata lunch na Rais wa Zanzibar, Mhe Dr Hussein Mwinyi, na Mama Anna Mkapa pale Lupaso. Jioni, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alipata dinner na Bw. William Erio na mkewe Janet huko Migongo, Masasi.

27. Mafanikio
Ile miaka miwili (1990-1992), Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, akiwa Askofu Mkuu Mwandamizi, ilibidi waandae bajeti na kuomba msaada kwa Wakapuchini kule Uswisi waone wanawezaje kusaidia.
Aliposhika madaraka, akawauliza waliokuwa kwenye uongozi kuwa je si fedheha kuomba fedha Uswisi kwaajili ya kununua mchele wa Kyela? Je, hawawezi kula mihogo?
Akaazimia kuwa vitu kama hivyo vinavyoweza kupatikana hapa nchini, wasiangaike kuombea fedha Uswisi kwani ni aibu kubwa. Akaona waamini kama hawana fedha wanaweza kusaidia kutoa mchele, Unga, ngombe, mbuzi, kuku nk.
Akasema wataomba fedha kwa vitu ambavyo kweli vinahitaji fedha. Akawashukuru Wakapuchini wa Uswisi kwa misaada yao na akasema wataomba fedha kwa vitu ambavyo viko nje ya uwezo wao tu. Hivyo, mwaka 1994, akaanzisha "Sera ya Tegemeza Jimbo" ambayo ilipata mafanikio makubwa.
Wazo lake la WAWATA ambalo alilitoa 1992 lilisaidia sana Visiga Junior Seminary. Pia, 2008, alianzisha UWAKA.
Aidha, alitoa mchango mkubwa kwenye kukataza mifarakano ya kidini baina ya Wakristu na Waislamu.
Pia, alipofika Dar es Salaam alikuta jimbo lina parokia 20 tu. Hivyo, mara kwa mara alikuwa akihamasisha na kuhubiri kuwa zifike 100. Hii ni kwasababu alitamani kuona waamini wa Dar es Salaam wanapata huduma za kichungaji kwa ukaribu zaidi. Hata hivyo, baadhi ya waamini waliona ni ndoto za mchana na walijiuliza kijana mdogo kama yeye alikuwa na miujiza gani ya kufanikisha hilo.
Wakati anamkabidhi Askofu Mkuu mpya wa jimbo la Dar es Salaam, Mhashamu Askofu Thaddeus Ruwa'ichi, alifurahi kuona ndoto yake imetimia kwani Jimbo lilikuwa na parokia 118.
Moja ya mifano mizuri ni Kanisa la Mtakatifu Yohane Paulo II lililoko Ununio. Siku moja mwaka 2010, Mwadhama Polycalp Kadinali Pengo alimkuta Mhe Paul Kimiti akisali kwenye Kigango, Ununio. Akampa jukumu la kuhakikisha wanajenga Kanisa. Mhe Kimiti akachakarika na wenzie kisha Mwadhama Polycalp Kadinali Pengo akawaongezea Tshs 45,000,000/= na sasa hilo ni miongoni mwa makanisa mazuri jimboni Dar es Salaam.
28. Changamoto
Katika utume wake, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alikumbana na changamoto lukuki. Miongoni mwa changamoto hizo ni:
28.1 Mparurano na CCM
Mwaka 2009, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alikwaruzana na chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alikuwa ametoa Taarifa kwa waamini jinsi ya kupata viongozi bora kwenye uchaguzi mkuu uliokuwa ukitarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2010.
NEC ya CCM ilichukizwa sana na katika kikao chake ikaja na Azimio kuwa Taasisi za dini lazma kwanza ziwasiliane na Serikali kabla ya kutoa Taarifa za aina hiyo.
Akiongea kwenye mazishi ya Mhashamu Askofu Anthony Mayalla siku chache baadaye, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alisema, kwa hisia kali, kuwa Kanisa halitawasiliana au kuomba ushauri kwa CCM au Serikali, itakapokuwa inawasiliana na waamini wake, aslan abadan ! Na kweli, Kanisa likaeendelea na utaratibu wake wa kawaida pasina vikwazo.
28.2 Mparurano na TEC
Mwaka 2014, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliivaa Kamati ya Amani & Usalama ya TEC iliyotoa Sekula iliyokuwa ikilitaka Bunge la Katiba lihakikishe mawazo ya Tume ya Warioba kuhusu mfumo wa Serikali tatu yanatekekezwa.
Siku mbili tu baadaye, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aling'aka na kudai maoni ya Kamati ya TEC hayawezi kuwa ndio msimamo wa Kanisa nchi nzima. Akafafanua kuwa Kanisa lina taratibu zake za kutoa Taarifa ambayo husainiwa na Rais wa TEC.
28.3 Mparurano na Askofu Gwajima
Mwaka 2015, Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima alimkashifu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na kuswekwa Lupango kwa kutoa lugha ya matusi na kashfa. Askofu Gwajima alikuwa amezomoka kama ifuatavyo:
"Mpuuzi mmoja, Mjinga mmoja anaitwa Askofu Pengo ambaye juzijuzi baada ya kula chakula chake, sijui amekula nini, anasema hovyohovyo! Mimi Gwajima namwita Mpuuzi yule, namwita Hafai yule, sijui amekula Maharage ya wapi Yule, Askofu Pengo sijui umezeeka wewe, haufai, Ondoka".
29. Tamati
Mwadhama Polycalp Kadinali Pengo alikuwa na wito wa kuwa Kiongozi wa dini. Alikuwa mwanafunzi hodari darasani na alijaliwa uwezo mkubwa wa kiakili wa kuweza kuchanganua mambo kisha kutoa uamuzi au ushauri wa hekima ndio maana alitwikwa majukumu makubwa akiwa na umri mdogo.
Wakati wa utume wake, aliwafinyanga Mapadri na Maaskofu wengi na alituliza madhoruba mbalimbali yaliyokuwa yakilikumba Taifa letu mf kati ya Kanisa na Serikali na Wakristu na Wasio Wakristu ndio maana Mhe Rais Samia alimtunukia Certificate of Recognition kwa kutambua mchango wake wa kipekee.
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ameacha asasi mbalimbali zitoazo huduma za elimu na afya jimboni na daima atakumbukwa.
Raha ya Milele Umpe Ee Bwana na Raha ya Milele Unwangazie Apumzike kwa Amani

Tunapatikana Kupitia